Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali ziongeze kodi kwenye bidhaa za tumbaku:WHO

Serikali ziongeze kodi kwenye bidhaa za tumbaku:WHO

Hadi sasa ni serikali chache zaidi duniani ambazo zinatoza kodi sahihi kwa sigara na bidhaa za tumbaku na hivyo kukosa fursa sahihi na iliyothibitishwa ya kudhibiti matumizi ya tumbaku. Taarifa zaidi na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika la afya duniani, WHO kuhusu magonjwa yatokanayo na matumizi ya tumbaku iliyochapishwa leo ikiangazia umuhimu wa kuinua kiwango cha kodi dhidi ya bidhaa za tumbaku.

Ripoti hiyo imezinduliwa leo huko Manila, Ufilipino, ambapo WHO inasema kuongeza kodi ni kipengele cha mwisho cha mkakati wa MPOWER uliomo katika mkataba wa kimataifa wa kudhibiti matumizi ya tumbaku.

Vinayak Prasad, meneja mradi wa udhibiti wa Tumbaku kutoka WHO anasema kuongeza kodi kunakumbwa na vikwazo kutoka kwa wafanyabiashara lakini ni vyema kutambua kuwa kwa kuongeza kodi..

(Sauti ya Dkt. Prasad)

“Mzigo wa gharama ya matibabu utapungua sana. Kodi zitaongeza sana mapato ambayo yatatumika kugharimia mipango mingine ya afya ya umma kama wajawazito na ile ya afya kwa wote. Inakadiriwa kuwa kodi itokanayo na tumbaku ni karibu dola bilioni 272 , hiyo ndiyo pesa ambayo tunalenga.”

Vipengele vingine ni kufuatilia matumizi ya tumbaku na sera za kinga ya matumizi, kulinda watu dhidi ya moshi wa tumbaku, kusaidia wanaotaka kuacha kuvuta sigara, kuonya watu kuhusu hatari za tumbaku na kusimamia marufuku za matangazo ya sigara.