Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubaguzi wa rangi na vitendo vya kutovumiliana vyamulikwa na Baraza la Haki za Binadamu

Ubaguzi wa rangi na vitendo vya kutovumiliana vyamulikwa na Baraza la Haki za Binadamu

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, leo limekuwa na mjadala kuhusu ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya wageni aina nyingine za kutovumiliana, pamoja na utekelezaji wa mpango wa kuchukua hatua ulioazimiwa mjini Durban, Afrika Kusini.

Mjadala huo umefanyika baada ya mazungumzo lililofanya baraza hilo na Mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya wageni na aina nyingine za kutovumiliana, Mutuma Ruteere.

Bwana Ruteere ameliambia baraza hilo kuwa ubaguzi mwingi unatokana na kuogopa wageni na hofu ya tishio la ugaidi na uhamiaji, akitaja mchango wa vyombo vya habari na mashirika ya umma katika kupambana na kutovumiliana, na umuhimu wa uwekaji takwimu na mafunzo kwa walinda sheria.

Wakati wa mjadala huo, waliohutubu wamelaani vitendo vyote vya kibaguzi kwa misingi ya rangi, wakisema kwamba vitendo hivyo hufanyika kila mahali, huku wakielezea hali katika baadhi ya nchi na mikakati iliyoanzishwa katika nchi zao ili kutekeleza kikamilifu azimio la Durban na mpango wa kuchukua hatua ili kuchagiza anuai ya kitamaduni na kikabila.