Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Safari ya mabadiliko ya tabianchi inatia moyo: Ban

Safari ya mabadiliko ya tabianchi inatia moyo: Ban

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao cha ngazi ya juu kuhusu mabadiliko ya tabianchi wakati huu ambapo miezi mitano kuanzia sasa dunia itapitisha mkataba mpya kuhusu suala hilo ambalo athari zake zinakuwa bayana kila uchao. Taarifa zaidi na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Safari ya kuchukua uamuzi jasiri kuhusu mabadiliko ya tabianchi imefikia wakati muhimu kabisa!

Amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alipoanza hotuba yake iliyosema kuwa mwelekeo wa safari hiyo unaonekana kutia moyo kwani hata nchi mbili zinazoongoza kwa utoaji wa hewa chafuzi ambazo ni China na Marekani pamoja na Muungano wa Ulaya wameshatangaza hatua za kudhibiti na nyingine zinafuatia..

Hivyo amesema ..

(Sauti ya Ban)

“Hebu na tukumbuke kila wakati kwamba mabadiliko ya tabianchi na maendeleo endelevu ni pande mbili za sarafu moja. Ajenda hizi mbili zinaimarishana:maendeleo ya upande mmoja yananufaisha upande mwingine kuanzia uhakika wa chakula hadi afya, nishati hadi maji na kukidhi mahitaji yote ya binadamu na jitihada zake. Maendeleo hayawezi kuwa endelevu iwapo hayashughulikia mabadiliko ya tabianchi.”

Mapema Rais wa Baraza Kuu Sam Kutesa akifungua kikao hicho amesema mabadiliko ya tabianchi ni dhahiri akisema yanaathiri wakulima maskini huko Uganda akitaka hatua zichukuliwe sasa bila kuchelewa.