Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAIDS yakaribisha ushahidi wa ziada kuhusu faida za kuanza ARV mapema

UNAIDS yakaribisha ushahidi wa ziada kuhusu faida za kuanza ARV mapema

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya Ukimwi, UNAIDS limekaribisha ushahidi wa ziada unaoonyesha kuwa kuanza matibabu ya dawa za ARV kinga ya mwili ikiwa bado ni thabiti kunachangia vyema afya na hali ya watu wanaoishi na virusi vya HIV.

Akikaribisha ushahidi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, Michel Sidibé amesema kila mtu anayeishi na HIV anapaswa kupata mara moja dawa za kuokoa maisha za ARV, akiongeza kwamba kutowezesha upatikanaji wa dawa hizo kwa kisingizio chochote ni kumnyima mtu haki ya kuwa na afya nzuri.

Utafiti mpya wa kimataifa kuhusu wakati wa kuanza matibabu ya ARV umeonyesha kuwa faida za kuanza mapema matibabu ya dawa za kupunguza makali ya kirusi cha HIV ni kubwa kuliko hatari zake.

Takwimu za utafiti huo zinaonyesha kuwa hatari ya kupata ugonjwa wa Ukimwi, magonjwa mengine hatari au kifo ilipunguzwa kwa asilimia 53 miongoni mwa watu walioanza matibabu wakati viwango vya kinga ya mwili au CD4 vikiwa 500 au zaidi, ikilinganishwa na wale waliochelewa na kuanza viwango vya CD4 vikiwa vimeshuka hadi 350.