Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtalaam wa UM aonya Marekani iwe makini katika matumizi ya drone

Mtalaam wa UM aonya Marekani iwe makini katika matumizi ya drone

Kundi la watalaam huru wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamekaribisha leo tangazo la Marekani kuangalia upya operesheni zao za kupambana na ugaidi kupitia ndege zisizo na rubani, yaani nyuki dume au drone kwa lugha ya kiingereza.

Wamesisitiza Marekani ihakikishe uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya ndege hizo.

Taarifa iliyotolewa leo na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu imesema kwamba Marekani imekiri kuuwa watu wanne kwa bahati mbaya wakati wa operesheni ya kupambana na ugaidi mpakani wa Afghanistan naPakistan.

Wataalam wa Umoja wa Mataifa wamekaribisha tangazo la rais Barack Obama wa Marekani la kuomba msamaha kwa familia za wahanga.

Aidha wameiomba serikali ya Marekani iondoe siri juu ya ripoti kuhusu operesheni hizo na kutangaza ni raia wangapi wameuawa kupitia ndege hizo.

Halikadhalika wataalam hao wa Umoja wa Mataifa wameeleza kwamba mamlaka za serikali zinaamua kutumia nyenzo hizo baada ya kupokea ripoti ambazo hazijadhibitishwa kikamilifu na kutathminiwa hivyo uchunguzi wahitajika zaidi kutambua uwajibikaji wa serikali katika vifo vya raia, wakiongeza kwamba uchunguzi huu unapswa kuwa huru na kufanyika kwa ngazi ya kitaifa na ya kimataifa.