Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto 800,000 walazimika kukimbia machafuko Nigeria na nchi jirani: UNICEF

Watoto 800,000 walazimika kukimbia machafuko Nigeria na nchi jirani: UNICEF

Ikiwa tarehe 14, Aprili, ni mwaka mmoja tangu kutekwa kwa wasichana Zaidi ya 200 watoto wa shule huko Chibok Nigeria , Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF linajikita katika athari za machafuko kwa watoto nchini humo. Amina Hassan na maelezo Zaidi.

(TAARIFA YA AMINA HASSAN)

Takriban watoto 800,000 wamelazimika kukimbia makwao kutokana na machafuko yanayoendelea Kaskazini Mashariki mwa Nigeria baina ya kundi la Boko Haram, majeshi ya serikali na makundi ya kiraia yaliyojihami kwa silaha imesema ripoti mpya ya UNICEF.

Ripoti hiyo iliyotolewa mwaka mmoja bada ya wasichana wa Chibok kutekwa inaonyesha kuwa idadi ya watoto wanaokimbia ili kuokoa maisha yao ndani ya Nigeria au kuvuka mpaka kuingia Chad, Niger na Cameroon imeongezeka Zaidi ya mara mbili kwa kipindi cha chini ya mwaka mmoja.

Kwa mujibu wa Manuel Fontaine mkurugenzi wa kanda ya Arika Magharibi na Kati wa UNICEF ,kutekwa kwa wasichana wa Chibok ni moja ya mika isiyokwisha na tatizo linaendelea katika sehemu mbalimbali za Nigeria.

Idadi kubwa ya wasichana na wavulana wamekuwa wakitoweka Nigeria kwa kutekwa, kuingizwa kwenye makundi yenye silaha, kushambuliwa, kutumiwa kama silaha au kulazimika kukimbia machafuko, suala ambalo linakiuka haki zao kama watoto.