Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sera thabiti na utashi wa kisiasa vyachochea elimu duniani:Ban

Sera thabiti na utashi wa kisiasa vyachochea elimu duniani:Ban

Wakati ripoti ya tathmini ya mwelekeo wa sekta ya elimu duniani kwa mwaka 2000-2015 ikizunduliwa duniani kote hii leo, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema uwezo wa vijana kujiendeleza hautakuwa na ukomo iwapo uwekezaji thabiti utafanyika katika sekta ya elimu.

Akitoa maoni yake kuhusu ripoti hiyo inayoangazia utekelezaji wa malengo Sita yaliyowekwa mwaka 2000 wakati wa kongamano la kwanza kuhusu Elimu lililofanyika Dakar Senegal, Katibu Mkuu amesema kumekuwepo na changamoto lakini kule ambako utashi ulikuwepo mafanikio yako dhahiri.

Mathalani watoto milioni 50 zaidi wako shule ya msingi na idadi ya watoto na vijana barubaru walio nje ya shule imepungua kwa asilimia 50.

"Tunafahamu maendeleo yanawezekana iwapo sera madhubuti zinakwenda sambamba na rasilimali zilizopo pamoja na utashi. Hili ni somo zuri kabia tunapoandaa ajenda ya maendeleo endelevu baada ya mwaka 2015 na kusongesha malengo ya mpango wa Elimu kwanza ili kila mtoto aende shule, kuhakikisha elimu bora na kuendeleza uraia wa dunia. Tunafahamu kuwa tunaposhirikiana na kuwekeza kwa mustakhbali wa baadaye, hakuna kitakachokwamisha vijana wetu kuchanua.”