Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kizuizini kunahusishwa na vitendo vya usumbufu, watoto ni lazima walindwe:Mtaalam

Kizuizini kunahusishwa na vitendo vya usumbufu, watoto ni lazima walindwe:Mtaalam

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya utesaji , Juan E. Mendez leo amezitaka serikali kupitisha sheria mbadala za zile za kuwaweka watoto kizuizini ambazo zitazingatia maslahi ya watoto na wajibu wa serikali wa kuwalinda watoto hao dhidi ya utesaji na usumbufu mwingine.

Amesema uwekaji watoto kizuizini kunahusiana na usumbufu kwa watoto na unyanyaswaji hasa katika hali ambazo zinawaweka watoto katika hatari ya kuonewa. Bwana Mendez ameyasema hayo wakati akiwasilisha ripoti yake kwenye baraza la haki za binadamu.

Amesema serikali zina wajibu wa kuchukua hatua za ziada kuhakikisha haki za watoto za kuishi, afya, utu wao, kutozurika kimwili na kiakili zinalindwa, lakini ameongeza kuwa mara nyingi hatua za kushughulikia ukiukaji huo wa haki zinakuwa hazitoshelezi.

Mtaalamu huyo wa haki za binadamu amesema kuwanyima watoto uhuru inatakiwa kuwa ni suluhisho la mwisho, na litumike tuu kwa muda mfupi, na kama ni kwa manufaa ya mtoto, kwa kesi maalumu.