CERF yatoa dola milioni 100 kwa operesheni za kibinadamu

23 Januari 2015

Mkuu wa masuala ya kibinadamu katika Umoja wa Mataifa, Valerie Amos, ametenga dola milioni 100 kutoka kwa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Shughuli za Dharura, CERF, kwa ajili ya kusaidia katika huduma za kuokoa maisha nchini Syria na katika nchi nyingine 11 ambako mahitaji ya kibinadamu ni makubwa lakini zinapokea usaidizi mdogo wa kifedha.

Bi Amos amesema licha ya kuwepo uhaba wa ufadhili, wahudumu wa kibinadamu wamejitoa kumsaidia kila raia wa Syria asiyejiweza. Amesema fedha hizo zilizotengwa kutoka CERF zitasaidia kuhakikisha kuwa wanaendelea na kazi yao hiyo.

Amesema katika kipindi chini ya miaka minne, idadi ya watu wanaohitaji usaidizi wa kibinadamu nchini Syria imepanda kutokamilioni moja hadi milioni 12, huku mamilioni ya wengine zaidi wakiwa wamekimbilia nchi zingine.

Dola zipatazo milioni 77.5 zitakwenda kusaidia kufadhili awamu za kwanza mbili za ufadhili wa CERF mwaka huu wa 2015 katika usaidizi wa dharura kwa nchi zilizoathiriwa na mzozo wa Syria, zikiwemo Misri, Iraq, Jordan, Lebanon na Uturuki.

Dola milioni 14 zitakwenda katika kusaidia operesheni za kibinadamu katika nchi tatu za ukanda wa Maziwa Makuu Afrika, zikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC ($9 milioni), Burundi ($2.5milioni) na Rwanda ($2.5 milioni), ili kuwasaidia watu waliolazimika kukimbia machafuko nchini DRC.

Nchi nyingine ambako wadau wa kibinadamu watapokea fedha za CERF ni Colombia ($3 milioni), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea ($2 milioni) na Djibouti ($3 milioni).

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter