Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNMEER azuru kituo cha tiba dhidi ya Ebola Sierra Leone

Mkuu wa UNMEER azuru kituo cha tiba dhidi ya Ebola Sierra Leone

Mwakilishi maalum wa katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mkuu wa ujumbe wa umoja huo unaoshughulikia dharura ya Ebola, UNMEER, Ismail Ould Chiekh Ahmed ametembelea kituo cha tiba dhidi ya Ebola kaskazini mwa Sierra Leone.

Kituo hicho kiitwacho Magbentah chenye uwezo wa kulaza wagonjwa 100 kinafadhiliwa na Muungano wa Afrika, AU na kinatajwa kuwa na idadi kubwa ya watu waliopona ugonjwa huo wa Ebola.

Akizungumza baada ya ziara Bwana Ahmed amesema amefurahi kuona kazi nzuri inayofanywa na wataalamu hao ambao wameshatibu wagonjwa 157 ambapo kati yao 101 wamepona.

Wakati wa ziara ya mkuu huyo wa UNMEER kulikuwepo na wagonjwa watatu tu ambapo Mratibu wa kituo hicho Dkt. John SSentanu amesema kutokana na kupungua kwa wagonjwa wa Ebola, sasa wataanza kutibu magonjwa mengine kwa wale watakaofika kituoni na kubainika hawana Ebola.

Wafanyakazi wa kituo hicho wakiwemo wataalamu wa magonjwa, wahudumu wa afya, wataalamu wa mawasiliano kwa umma na wa afya ya umma wanatoka Nigeria, Uganda, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Ethiopia.