Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lapongeza kujisalimisha Ntaganda ICC

Baraza la Usalama lapongeza kujisalimisha Ntaganda ICC

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limesifu kitendo cha mtuhumiwa wa uhalifu wa kivita Bosco Ntaganda kujisalimisha kwenye mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC huko The Hague tarehe 22 mwezi huu huu. Taarifa ya baraza hilo imekariri wajumbe wakipongeza nchi zilizofanikisha hatua ya kujisalimisha kwa Ntaganda na kusema kuwa kitendo hicho kinaashiria hatua chanya za kupatikana kwa haki na pia kurejeshwa kwa amani na usalama huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, DRC. Hata hivyo wajumbe wameonyesha wasiwasi wao juu ya kuendelea kuwepo kwa vitendo vya ukatili na ukiukwaji wa haki za binadamu Mashariki mwa DRC na kukumbusha kuwa wote wahusika wa vitendo hivyo wanapaswa kuwajibishwa. Wametaja baadhi ya watuhumiwa ambao bado wanasakwa kwa tuhuma za ukiukwaji huo kuwa ni pamoja na Sylvestre Mudacumura, mkuu wa kikundi cha FDLR.  Wajumbe wamerejelea wajibu wa nchi wanachama kwa mujibu wa mfumo wa kuwekea vikwazo wahusika kama ilivyopatiwa msisitizo kwenye azimio namba 2078 la Baraza la Usalama.