Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 18,000 wathibitishwa kuhama makwao Darfur Kaskazini

Watu 18,000 wathibitishwa kuhama makwao Darfur Kaskazini

Zaidi ya watu 18,000 wamethibitishwa kulazimika upya kuhama makwao kwenye maeneo ya El Fasher, Shangil Tobaya, Tawila na Um Baru Darfur Kaskazini, kwa mujibu wa wadau wa kibinadamu.

Ofisi ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura, OCHA, imesema zaidi ya watu 2,200 kati ya wale waliofurushwa makwao wanahifadhiwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika, UNAMID, kwenye kituo chake cha Um Baru, Darfur Kaskazini, ambako watu wengine wanaendelea kuwasili wakitafuta makazi na ulinzi.

Mashirika ya kutoa misaada yanaendelea kutoa usaidizi, ukiwemo huduma za afya na vifaa vya matumizi ya nyumbani, huku mipango ikifanyika ya kuwapa vifaa vingine, vikiwemo maji, vya kujisafi na lishe.

OCHA imsema watu wapatao 200 wamewasili pia kwenye kituo kingine cha UNAMID, Sortony, wakihofia vijiji vyao kushambuliwa, lakini inasemekana wahudumu wa kibinadamu wanapata ugumu kukifikia kituo hicho kilichotengwa. Juhudi zinafanywa ili kufanya tathmini ya mahitaji na kupeleka misaada ya kibinadamu.