Tutumie fursa iliyopo kutatua mzozo huko Sahel: Ban

Tutumie fursa iliyopo kutatua mzozo huko Sahel: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon na Rais wa Benki ya dunia, Jim Yong Kim wiki ijayo wataanza ziara kwenye ukanda wa Sahel barani Afrika ambapo watafanya ziara huko Mali, Niger, Burkina Faso na Chad.  Akitangaza ziara hiyo kwa waandishi wa habari mjiniNew York siku ya Ijumaa, Ban amesema ziara hiyo kwenye eneo hilo lenye hali ngumu ya kiuchumi na kijamii inalenga kutumia fursa ya matumaini iliyojitokeza kutokana na jitihada za pamoja baada ya mzozo ulioleta madhara. Amesema nchini Mali yahitajika juhudi madhubuti kuondoa matatizo yanayochochea mapigano badala ya kutumia mfumo wa zimamoto, na pili mtazamo wa kikanda ni muhimu kwa kuwa mzozo wa Sahel hautambui mipaka. Amesema eneo hilo linakabiliwa na ukame, ugaidi, uhalifu na hata ukosefu wa uhakika chakula ambapo watoto Milioni Nne wenye umri wa chini ya miaka mitano wako hatarini kupata utapiamlo.

(sauti ya Ban)

 “Changamoto hizi haziwezi kukabiliwa na serikali au taasisi moja pekee. Haya masuala yanaunganika na tunahitaji jitihada za pamoja. Mkakati wa Umoja wa Mataifa kwa Sahel ndio unafanya hivyo. Unaweka kipaumbele kwa utawala bora, ulinzi na ujasiri. Unasisitiza haki za binadamu na fursa kwa wanawake na vijana. Viongozi wa Sahel wanaugana kushughulikia changamoto hizi kwa pamoja. Wanahitajia msaada wetu. Ujumbe wetu kwenye ziara hii muhimu na kwa dunia nzima ni kwamba amani na maendeleo ni lazima viende pamoja.”

Katika mkutano huo na waandishi wa habari Rais wa Benki ya dunia alizungumza kwa njia ya video kutoka Washington D.C na kusema ziara hiyo ni muhimu kwa kutoa fursa mbali mbali za kumaliza umaskini kupitia ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi kama ambavyo ziara yao ya mapema mwaka huu huko Ukanda wa maziwa makuu Afrika ilivyoanza kuleta matumaini.  Wakati wa ziara hiyo huko Sahel, wataungana pia na viongozi kadhaa akiwemo Mwenyekiti wa  Tume ya Muungano wa Afrika Nkosazana Dlamini-Zuma na Rais wa Benki ya maendeleo ya Afrika Donald Kaberuka, Kamishna wa maendeleo wa Umoja wa Ulaya na mjumbe maalum wa Katibu Mkuu huko Sahel, Romano Prodi.