Usafirishaji haramu wa watoto unaongezeka- ripoti ya UNODC

24 Novemba 2014

Vitendo vya usafirishaji haramu wa watoto vinaongezeka kote duniani, kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa leo Jumatatu na Umoja wa Mataifa. Taarifa kamili na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grece)

Ripoti hiyo ya mwaka 2014 kuhusu usafirishaji haramu wa watu duniani, inaonyesha kuwa kati ya kila waathiriwa watatu wa usafririshaji haramu, mmoja ni mtoto- ikionyesha ongezekeo la asilimia 5, ikilinganishwa na kipindi kati ya mwaka 2007 na 2010.

Wasichana wanaathiriwa zaidi, wakichangia wawili kati ya kila watoto watatu wanaosafirishwa, na hivyo kuchangia idadi nzima ya wanawake kuwa asilimia sabini ya watu wanaoathiriwa na vitendo vya usafirishaji haramu wa watu duniani.

Ripoti hiyo ambayo imetolewa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Madawa na Uhalifu, imeonya kuwa hakuna nchi iliyo na kinga dhidi ya vitendo hivi, na kwamba kuna nchi zipatazo 152 wanakotoka waathiriwa wa uhalifu huo, huku nchi wanakoishia zikiwa ni 124.

Ripoti inaongeza kuwa usafirishaji haramu wa watoto ni tatizo kubwa katika maeneo fulani, kama vile Afrika na Mashariki ya Kati, ambako asilimia 62 ya waathiriwa wanatoka.

Ripoti hiyo pia inaeleza mchango wa uhalifu wa kupanga katika usafirishaji haramu wa watu.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter