Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu bilioni 2.2 ni maskini au waelekea kuwa maskini- ripoti ya UNDP

Picha: UNDP/DRC

Watu bilioni 2.2 ni maskini au waelekea kuwa maskini- ripoti ya UNDP

Ripoti mpya kuhusu maendeleo ya mwanadamu imeonya kuwa, umaskini na utaka wa mara kwa mara ni tishio kwa maendeleo ya mwanadamu, na usipokabiliwa ipasavyo kwa sera na kanuni za kijamii, hakutakuwa na maendeleo kwa njia ya usawa na endelevu.

Taarifa ya John Ronoh

Ripoti ya maendeleo ya mwanadamu ya mwaka 2014, imezinduliwa leo mjini Tokyo, Japan na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzō Abe, Msimamizi wa Shirika la Mpango wa Maendeleo, Helen Clark, na Mkurugenzi wa Ofisi ya Ripoti ya Maendeleo ya Mwanadamu, Khalid Malik. Bwana Malik anaeleza kuhusu ripoti hiyo.

Ripoti hiyo inaangazia jinsi ya kudumisha maendeleo ya ubinadamu kwa kupunguza utaka na kuimarisha ustahimilivu katika nyakati ngumu.

Kwa mujibu wa vipimo vya umaskini vinavyoangazia vipato vya watu, watu wapatao bilioni 1.2 wanaishi kwa dola 1.25 au chini ya kiasi hicho kila siku.  Hata hivyo, makadirio ya hivi karibuni zaidi ya UNDP yanabainisha kuwa takriban watu bilioni 1.5 katika nchi 91 zinazoendelea wanaishi katika ufukara, wakiwa na uhaba wa huduma za afya, elimu na, kuwa kwenye viwango vya chini vya maisha.

Ripoti inaonyesha kuwa ingawa umaskini unapungua, takriban watu milioni 800 wamo hatarini kutumbukia tena kwenye umaskini ikiwa watakabiliwa na majanga.