Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali ni mtumishi wa wananchi na si vinginevyo: Kamishna Zeid

UN Photo/Paulo Filgueiras
Kaminshna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Mwanamfalme Zeid Ra’ad Hussen. Picha:

Serikali ni mtumishi wa wananchi na si vinginevyo: Kamishna Zeid

Kamishna mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein amesema majanga mengi yanayoendelea duniani hivi sasa kuanzia mapigano hadi magonjwa yatapatiwa suluhu iwapo haki za binadamu zitazingatiwa.

Akitoa ripoti ya utekelezaji ya ofisi yake kuanzia Agosti 2013 hadi Julai mwaka huu mbele ya Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Kamishna Zeid ametolea mfano mapigano yanayosababisha vifo huko Syria, Iraq, Sudan Kusini bila kusahau janga la Ebola.

Amesema kila pande inalalamika lakini ni vyema kufahamu kuwa msingi wa kutokomeza hayo yote ni kuzingatia haki za binadamu.

(Sauti ya Kamishna Zeid)

“Ndani ya chumba hiki, kama ilivyo kwenye vyumba vingine, wawakilishi kutoka nchi nyingi mara kwa mara wanarudia hofu yao juu ya haki za binadamu. Lakini ni lazima ieleweke vyema kwenu nyote kuwa njia pekee ya kuepuka majanga ni kuchukua hatua halisia za kuzingatia haki za binadamu ambazo nchi zote zimeazimia kuheshimu.”

Katika ripoti yake pia ameeleza masikitiko yake juu ya vitisho vya mara kwa mara dhidi ya watetezi wa haki za binadamu ambao wanafanya kazi ya kishujaa lakini wanakandamizwa.

(Sauti ya Kamishna Zeid)

“Iwapo licha ya nguvu na mamlaka zote iliyo nayo, hatma ya serikali inategemea ujumbe kwenye twitter au maandamano, au ripoti muhimu ya NGO au Umoja wa Mataifa, basi serikali hiyo iko kwenye matatizo makubwa kuliko inavyooamini, kwa kuwa imesahau msingi muhimu kuwa serikali ni mtumishi wa wananchi na si vinginevyo.”