Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Syria sasa yatosha, pande husika afikianeni: China

Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi. (Picha:UN /Kim Haughton)

Syria sasa yatosha, pande husika afikianeni: China

Waziri wa Mambo ya nje wa China Wang Yi, amehutubia mjadala Mkuu wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa akigusia masuala ya amani na usalama duniani, mabadiliko ya tabianchi na maendeleo endelevu.

Kuhusu Syria amesema ni mwaka wa nne sasa tangu kuanza kwa mzozo huo ambaoe umesababisha machungu kwa raia akitanabaisha suluhu itapatikana siyo kupitia vita bali mazungumzo.

Amesema pande zote husika zifuate mwelekeo wa mazungumzo kama yanavyoelekezwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ili kuleta suluhu ya kisiasa na ya kudumu kwenye mzozo huo.

Akizungumzia mabadiliko ya tabianchi Waziri Wang amesema hiyo ni changamoto ya aina yake kwa binadamu na ni matumaini yake kuwa kasi ya kisiasa iliyoonyeshwa wakati wa mkutano wa tabianchi utageuzwa kuwa wa vitendo zaidi ili mwakani kupatikane makubaliano ya dhati kuhusu tabianchi.

Ikiwa ni chini ya mwaka mmoja kabla ya ukomo wa malengo ya milenia, Waziri Wang amesema China ingalipenda kuona malengo ya maendeleo endelevu yanakuwa matatu.

Ameyataja kuwa ni kusongesha mbele ustawi wa wananchi kwa kutokomeza umaskini, pili kupatia kipaumbele kuendeleza ujumuishi ili kufikia haki ya kijamii na tatu ihakikishe utekelezaji.

Waziri Wang ametaka malengo hayo yaongozwe na msingi wa uwajibikaji unaozingatia fursa tofauti zinazokabili kila nchi.