Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mchango wa wanawake katika maendeleo ni dhahiri lakini bado kuna vikwazo: UM

Mchango wa wanawake katika maendeleo ni dhahiri lakini bado kuna vikwazo: UM

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN-Women limeanda kongamano la ngazi ya juu kuhusu siku ya wanawake duniani likimulika maudhui ya mwaka huu Usawa kwa wanawake ni maendeleo kwa wote.

Miongoni mwa washiriki alikuwa Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa John William Ashe, ambaye amesema hatua zimepigwa za kusherehekewa tangu Siku ya Wanawake ilipoadhimishwa kwanza na Umoja wa Mataifa mnamo mwaka 1975. Amesema mchango wa wanawake katika maendeleo endelevu ni dhahiri.

“Sote tunajua kwamba hatutaweza kutokomeza umaskini ulokithiri bila kuwashirikisha kikamilifu wanawake ambao ni nusu ya idadi ya watu duniani. Wanawake, wawe wanapoendesha biashara, kufanya kazi shambani au kubeba maji na kuhudumia watoto na watu wazima, juhudi zao hazifaidi tu familia zao, lakini zinanufaisha pia jamii zao” 

Naye Katibu Mkuu Ban Ki-Moon amesema kote duniani, ubaguzi dhidi ya wanawake bado umeenea, ingawa ni dhahiri kuwa usawa kwa wanawake ni maendeleo kwa wote.

“Nchi zenye usawa zaidi wa jinsia zina maendeleo zaidi kiuchumi, kampuni zenye wanawake zaidi kwenye bodi zao, zina faida zaidi, mikataba ya amani inayoshirikisha wanawake, hufanikiwa zaidi; Mabunge yenye wanawake zaidi, humulika masuala mengi zaidi, yakiwemo afya, elimu, kupinga ubaguzi na kuwasaidia watoto” 

Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani wa Marekani Bi Hillary Clinton, amesema wanawake wanaposhinda, ulimwengu unashinda, na hivyo ajenda mpya ya maendeleo ni lazima iwe jumuishi.

“Ni lazima tuhakikishe kuwa wanawake popote pale wana haki ya kupata ajira, kumiliki na kurithi mali, waweze kuwa utambulisho rasmi na halali, usawa katika elimu, wawe na washiriki kama wadau katika ujenzi wa amani, kutokomeza ukatili wa kijinsia, na pia ndoa za utotoni.” (Grace)

Mkuu wa kitengo cha Wanawake katika Umoja wa Mataifa, Phumzile Mlambo-Ncguka, amesema usawa baina ya wanawake na wanaume ni ndoto ambayo bado inakwepwa…

(Sauti ya Phumzile)

Sura ya umaskini ni ile ya mwanamke, idadi kubwa ya wajinga wa kutokujua kusoma na kuandika duniani ni wanawake na wasichana. Mwanamke mmoja kati ya watatu kwenye nchi maskini au tajiri duniani atakumbwa na ukatili wa vipigo au kingono katika maisha yake. Mamilioni ya wanawake na watoto wanauzwa utumwani. Lakini matatizo yote haya yana majibu! Majibu ni kuwawezesha wanawake, na majibu yako mikononi mwetu sote.”