Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Akiwa ukingoni kuhitimisha muda wake, Ashe azungumzia kilichomkatisha tamaa

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa John Ashe wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, tarehe 10 Septemba 2014. (Picha:UN /Mark Garten).

Akiwa ukingoni kuhitimisha muda wake, Ashe azungumzia kilichomkatisha tamaa

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa litakuwa na kikao cha siku mbili cha kutathmini mwelekeo wa mchakato wa ajenda ya maendeleo endelevu baada ya mwaka 2015 kabla ya kuanza kwa mkutano wa 69 wa Barazahilobaadaye mwezi huu.

Kikao hicho cha Alhamisi na Ijumaa kimeitishwa na Rais wa Baraza hilo John Ashe ambaye amewaambia waandishi wa habari kuwa wakati wa vikao wawakilishi wa nchi wanachama watakuwa na fursa ya kupitia ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon yenye mapendekezo ya ajenda hiyo kutoka kwa wadau mbali mbali.

(Sauti ya Ashe)

“Kwa hiyo lengo la mkutano wa kesho ni kutoa fursa kwa nchi wanachama kubadilishana mawazo na kwa Katibu Mkuu na wafanyakazi wake kusikiliza maoni na michangao ya wanachama na kile ambacho wangalipenda kijumuishwe kwenye ripoti. Ripoti hiyo siyo mwongozo wa kudumu.”

Rais huyo wa Baraza Kuu amesema wakati wa mkutano, washiriki watakuwa na fursa ya kuchangia maoni yao ili kuboresha ripoti hiyo ambayo itakuwa msingi wa majadiliano ya ajenda hiyo wakati wa mkutano wa 69 kabla ya kupitishwa na baraza hilo mwezi Septemba mwakani.

Bwana Ashe ambaye anamaliza muda wake wa kuongoza baraza kuu tarehe 15 mwezi huu, akaulizwa swali na mwandishi mmoja wa habari ni jambo gani lilimkatisha tamaa..

(Sauti ya Ashe)

"Marekebisho ya muundo wa baraza la Usalama ni hoja ngumu, na kila rais wa Baraza kuu huwa na matumaini kabisa mwanzoni kuwa anaweza kuleta mabadiliko. Lakini ni vyema kutambua kuwa hoja hiyo itabakia ni kiulizo hadi pale nchi wanachama zitakapokubaliana juu ya mfumo wa marekebisho Kwa hiyo tutakuwa na suala la usalama, lakini hatutaweza kufanya marekebisho ya muundo. Na kwangu mimi, ijapokuwa nilidhani nimefanya mambo makubwa, kushindwa kupata mafanikio makubwa kusongesha ajenda hiyo kumenikatisha tamaa.”

Hata hivyo amesema kinachomtia moyo ni kutimia kwa azma yake ya kuwepo kwa nyaraka za maandalizi ya ajenda ya maendeleo endelevu baada ya mwaka 2015 pamoja na kukamilika kwa maandalizi ya mkutano dunia wa watu wa asili tarehe 22 mwezi huu mjini New York.