Ban ataka nchi nane ziridhie mkataba dhidi ya majaribio ya nyuklia

29 Agosti 2014

Majaribio ya nyuklia kuanzia lile la Urusi la mwaka 1945 na mengine 455 yaliyofuatia baada ya hapo yamekuwa na madhara makubwa kwa binadamu na mazingira yanayowazunguka na hivyo ni lazima tujizatiti kuondokana na majaribio hayo.

Ni sehemu ya ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon katika siku ya kimataifa ya kupiga marufuku majaribio ya nyuklia tarehe 29 Agosti.  Ban amesema majaribio hayo yamekuwa alama ya harakati za kuendeleza silaha za nyuklia na kuhatarisha uwepo wa binadamu wote wale wanaotengeneza na wale zinazotumiwa dhidi yao.

Ametolea mfano wahanga wa mashambulio ya Hiroshima, Nagasaki na Semipalatinski akisema katika ziara zake amekutana nao na kuona vile walivyoazimia kuona dunia bila silaha hizo.

Kwa mantiki hiyo Ban ametaka siku ya leo iwe kichocheo cha kila mtu kuwa na mtazamo kama wa  manusura wa mashambulio ya nyuklia akisema kuwa hilo litawezesha kubadili msimamo unaofanya baadhi kuendeleza silaha hizo.

Katibu Mkuu ametaka nchia ambazo hazijaridhia mkataba wa kimataifa wa kutokomeza silaha za nyuklia zifanye hivyo ili uanze kutumika.  Akizungumzia suala la silaha za nyuklia, Katibu Mtendaji wa shirika linalosimamia utekelezaji wa mkataba huo, CTBTO, ,Lassina Zerbo anasema..

(Sauti ya Zerbo)

"Tunapaswa kuhakikishia nchi ambazo usalama wa Taifa unategemea usalama wa kimataifa na zile ambazo usalama wa kimataifa unategemea usalama wa kitaifa. Mashariki ya Kati nchi jirani zinatizamana! China inatizama Marekani na Marekani inatizama nyininezo. Hivyo nimewaeleza mawaziri wa kigeni wa kila nchi ambao nimekutana nao waonyeshe uongozi. Iwapo China na Marekani zitaridhia, hii itaweka muundo wa kuiaminiana. Lakini tunaona nchi hizo nane zote kuwa ni sawa na tunafikiri kitendo cha kuridhia kitakachofanywa na yoyote kati yao kitaweka imani katika muundo tunaohitaji ili mkataba uweze kutumika. "

Nchi hizo ni Nane ni China, Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Korea, Misri, India, Iran, Israel, Pakistan na Marekani.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter