Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa watiwa wasiwasi na hali ya usalama Iraq kaskazini

Wakimbizi kutoka Mosul waliotafuta hifadhi Kurdistan @UNHCR/ S. Baldwin

Umoja wa Mataifa watiwa wasiwasi na hali ya usalama Iraq kaskazini

Umoja wa Mataifa umesema una wasiwasi sana kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama na ya kibinadamu kaskazini mwa Iraq.

Naibu Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Gyorgy Busztin amesema hali hiyo inatokana na kwamba kundi la waislamu wenye msimamo mkali la ISIL na waasi wengine wamevamia maeneo ya Ninewa, na mapigano yanaendelea hadi sasa mpakani mwa mkoa wa Kurdistan na jeshi la Kikurdi.

Amesema kwa kipindi cha siku mbili, zaidi ya watu 200,000 wamekimbia makwao kutokana na mapigano.

Wengine karibu 200,000 wenye asili ya Kiyezidi wametegwa kwa kipindi cha siku tano kwenye eneo la mlima wa Jabal Sinjar, hasa wanawake na watoto, ambapo wamekosa huduma zote za kibinadamu, hasa maji ya kunywa. Idadi kubwa ya waliokimbia ni watu kutoka makundi madogo ikiwemo wakristo, washabak na wayezidi.

Busztin amesema Umoja wa Mataifa unaendelea kupata ripoti za ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwemo watu kuuawa, kubadilishwa dini kwa nguvu, kubakwa, na kubomolewa kwa sehemu zao za ibada, vyote vikilenga kuondoa vikundi vyote visivyo vya Wasunni katika eneo hilo.

Kwa mantiki hiyo ameziomba serikali ya Iraq na ya mkoa wa Kurdistan kushirikiana ili kuwasaidia wakimbizi hao, akiiomba pia jamii ya kimataifa kuzisaidia serikali hizo katika shughuli za kuwapatia wakimbizi misaada ya kibinadamu, na kuwalinda na ukiukwaji wa haki za binadamu.