Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchaguzi wa 2015 utakuwa mtihani wa demokrasia kwa Burundi

Mkuu wa BNUB, Parfait Onanga Anyanga, @UNphotos

Uchaguzi wa 2015 utakuwa mtihani wa demokrasia kwa Burundi

Ingawa serikali ya Burundi inajitahidi kujenga mazingira ya utulivu kabla ya uchaguzi mkuu mwaka 2015, mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo Parfait Onanga-Anyanga amesema bado hali ya kisiasa ni ya sintofahamu baina chama tawala na vile vya upinzani.

Aliwaeleza wajumbe wa Baraza la Usalama siku ya jumatano, kuwa bado hakuna mazungumzo huru kuhusu maswala mengi ya kisiasa ya kitaifa, na watu wamekuwa na wasiwasi kutokana na baadhi ya sheria zilizopitishwa zinazozuia haki ya kujieleza huru au kuandamana.

Hata hivyo, amesema, zipo sababu za kutia moyo, mathalani Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza ambaye amewataka mawaziri wake wahakikishe vyama vya upinzani vinaendelea na shughuli zao kwa uhuru.

Bwana Onanga-Anyanga amekaribisha pia tamko la mwenyekiti wa chama tawala, CNDD-FDD la kulaani ghasia zilizotekelezwa na vijana wa chama tawala likieleza kuwa watafikishwa mbele ya sheria. Hivyo amesema kuna matumaini.

“ Siku ya Julai mosi, Rais Nkurunziza alitangaza uchaguzi wa 2015 utakuwa uchaguzi bora ulioandaliwa nchini humo. Juu ya hayo, vyama vya upinzani vimeendelea kushirikiana kwenye mazungumzo ya kisiasa, na vimeamua kutosusia uchaguzi wa 2015. Inatia moyo sana, kwani uchaguzi wa 2015 utakuwa mtihani wa kweli wa Burundi kwa demokrasia na utulivu.”