Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yaendelea kufuatilia mkurupuko wa Ebola Afrika Magharibi

Muuguzi akimuhudumia mgonjwa mwenye virusi vya Ebola. WHO/Chris Black

WHO yaendelea kufuatilia mkurupuko wa Ebola Afrika Magharibi

Shirika la afya duniani WHO, linajitahidi kufuatilia kwa makini hali ya mlipuko wa virusi vya Ebola katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone. Nchini Guinea, kuenea kwa virusi kumepungua kwa kiasi kikubwa, na kisa kimoja tu kimeripotiwa kwa siku 7 zilizopita.

WHO inaendelea kufuatilia hali kwa makini hasa ikilenga jamii ambazo zilikuwa zimepuuza mapendekezo ya kuzuia kuenea kwa virusi katika makazi yao. Wakati huo huo, viwango vya maambukizi nchini Liberia na Sierra Leone bado viko juu kwa sababu kumekuwa na visa vipya vya maambukizi na pia vifo vimeripotiwa.

Kwa mujibu ya wizara za afya za nchi hizo mbili, sehemu za Kailahun na Kenema nchini Sierra Leona, na Lofa na Montserrado nchini Liberia ndizo zilizoko hatarini baada ya mkurupuko kuzuka. Wizara za Afya za nchi hizo zinashrikaian na WHO ili kudhibiti hali hiyo.

Daktari Keiji Fukuda wa Shirika la Afya Duniani ametoa kauli ya shirikia hilo kwamba, njia ya kudhibiti hali ya uenezaji ya virusi hivyo ni kuwahusisha wadau wote kwa majadiliano ili kuwa na maafikiano thabiti ya kupambana na tatizo la Ebola.

Kituo cha kuratibu maswala ya mkurupuko katika ukanda huo wa Afrika Magharibi kimeanzishwa jijini Conakry, Guinea. Kituo hicho kitawezesha ushirikiano, uhamasishaji na juhudi za dharura ili kukabiliana na janga hilo la Ebola mara tu linapoibuka.

Shirika la Afya Duniani kwa sasa halijatoa ushauri wa kuzuia usafiri ya watu na bidhaa kwa nchi hizo za Guinea, Liberia au sierra Leone.