Nchi za Ulaya zaombwa kuwasaidia wasaka hifadhi wa Syria
Nchi za bara Ulaya zimehimizwa kufungua milango kwa wakimbizi wa Syria na kuwapa utaratibu sahihi wanaosaka hifadhi. Wito huo umetolewa na Shirika la kuhudumia Wakimbizi Duniani, UNHCR wakati wa uzinduzi wa ripoti kuhusu hali ya wakimbizi wa Syria walioko Ulaya.
UNHCR imeyaomba mataifa hayo kuwapokea vilivyo na kuwalinda wakimbizi hao wanaokimbia mzozo nchini Syria. Shirika hilo kupitia msemaji wake limesema kwamba Idadi kubwa ya wakimbizi wa Syria wanakimbilia nchi zilizoko mbali na eneo lao na hivyo kuchukua safari ndefu na hatari wakitafuta hifadhi. Wengi wa wakimbizi hao wana jamaa Ulaya na nia yao ni kuunganishwa nao.
Kadhalika UNHCR imesema kwamba tangu mzozo wa Syria ulipoanza Mwezi Machi 2011, wakimbizi 123,600 wametafuta hifadhi nchi za Ulaya ikilinganishwa na wakimbizi milioni 2.9 waliokimbilia nchi jirani. Kufikia sasa nchi za bara Ulaya zimewapatia hifadhi takriban wakimbizi 32,000 wa Syria.