Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jukwaa la kimataifa la elimu lichochee elimu ya kustahimiliana: Ban

Jukwaa la kimataifa la elimu lichochee elimu ya kustahimiliana: Ban

Jukwaa la tatu la kimataifa kuhusu elimu litakalofanyika mwezi Mei mwaka huu huko Jamhuri ya Korea litakuwa na mchango mkubwa kwenye ajenda mpya ya maendeleo endelevu inayotarajiwa kupitishwa mwezi Septemba mwaka huu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema hayo kwenye kikao kilichofanyika New York, kupeana taarifa kuhusu maandalizi ya jukwaa hilo.

Amesema ni matarajio yake kuwa jukwaa litaibuka na jitihada za saa za ajenda hiyo inayotaka kuwepo kwa ajenda moja ya elimu inayonufaisha makundi yote.

Ban amesema hiyo ni muhimu kwani maeneo mbali mbali duniani, wasichana na wavulana wengi hawamalizi masomo kutokana na mizozo na majanga huku vijana wengine wakimaliza shule bila stadi sahihi za kuwakwamua kimaisha.

Halikadhalika amegusia pia kundi la watu wazim hususan wanawake akisema wengi ni wajinga wa kutokujua kusoma na kuandika kwenye zama za sasa za mapinduzi ya digitali.

(Sauti ya Ban)

“Tunahitaji mtazamo jumuishi na thabiti ya masomo kwa wote. Tangu mwaka 2000 kumekuwepo na maendeleo kwenye malengo ya milenia na elimu kwa wote. Kwa pamoja tuhakikishe hakuna anayebaki nyuma, kila mtu aende shule, anapta stadi mpya za mafunzo kwa ajili ya kuwa raia wa dunia.”

Ban amesema katika zama za sasa zilizoghubikwa na misimamo mikali na kutovumiliana ni vyema kuchagiza mafunzo ya uraia wa dunia yanayoweza kujenga jamii yenye kuvumiliana, kustahimiliana na kujenga maelewano.