Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Hapa na Pale

Baraza la Usalama limepitisha, Alkhamisi asubuhi, azimio liloruhusu kuongeza, kwa muda, vikosi vya wanajeshi wa MONUC ili kudhibiti vurugu na fukuto la mapigano yaliozuka kwenye eneo la mashariki, katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Mapigano katika eneo hilo la nchi yalisababisha raia 250,000 kung’olewa makazi katika miezi ya karibuni, umma ambao unategemea misaada ya dharura kutoka mashirika ya kimataifa ili kukidhi mahitaji ya kimsingi. Azimio limependekeza kupelekwe wanajeshi wa kimataifa 2,785 pamoja na vikosi vya askari polisi 300. ~

Mtaalamu Huru wa UM juu ya Haki za Binadamu ahadharisha mateso yamepamba vizuizini Guinea-Bissau

Manfred Nowak, Mkariri Maalumu wa UM juu ya Mateso na adhabu nyengine katili zinazodhalilisha utu, baada ya kumaliza ziara yake katika taifa la Guinea-Bissau, aliwaambia waandishi habari ya kwamba raia wanaojikuta kwenye vizuizi vya polisi katika taifa hilo [mara nyingi] huteswa na kusumbuliwa kwa mpangalio, na wakati huo huo wafungwa huadhibiwa kikatili kabisa, hali ambayo anaamini inasababishwa na kuharibika kabisa kwa mfumo wa sheria katika nchi. Alisema wafungwa wa kisiasa, pamoja na wale watuhumiwa wa uhalifu wa kawaida, wote huteswa na polisi katika Guinea-Bisaau, [pale wanaposhikwa na hulazimishwa] wakubali kukiri makosa bila ushahidi wala kupelekwa mahakamani.~~

Hapa na Pale

Leo Baraza la Usalama lilifanyisha majadiliano ya hadhara, yalioongozwa na Raisi Oscar Arias wa Costa Rica, taifa mwenyekiti wa shughuli za Baraza kwa mwezi Novemba. Majadiliano yalizingatia namna ya kuimarisha usalama wa pamoja, kwa kuandaa sheria ya jumla itakayotumiwa kupunguza silaha na zana za vita ulimwenguni, kwa makusudio ya kusawazisha usalama na kuimarisha amani ya kimataifa.

OCHA inasema wahamiaji 25,000 wamekusanyika katika kambi ya MONUC kuomba hifadhi

Ofisi ya UM Inayohusika na Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti watu 25,000 waliong’olewa makazi wamekusanyika kwenye kambi ya walinzi amani wa MONUC, ya Bambu, iliopo kilomita 80 kaskazini ya mji wa Goma kutafuta hifadhi na misaada ya kihali, kwa sababu kwenye jimbo lao kumekosekana mashirika ya kimataifa yanayohudumia misaada ya kiutu kwa waathiriwa wa vurugu liliopamba majuzi kwenye eneo lao.~~

Mapigano yawanyima wanafunzi 150,000 fursa ya kuilimishwa katika JKK: UNICEF

Veronique Taveau, Msemaji wa Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) aliwaambia waandishi habari wa kimataifa Geneva, ya kwamba kutokana na mapigano yaliotanda katika JKK, skuli kadha zimelazimika kufungwa katika eneo la Rutshuru, na ambayo wanafunzi 150,000 ziada wananyimwa fursa ya masomo, maana hali ni ya wahka mkubwa na ya hatari sana.