Hapa na Pale
Baraza la Usalama limepitisha, Alkhamisi asubuhi, azimio liloruhusu kuongeza, kwa muda, vikosi vya wanajeshi wa MONUC ili kudhibiti vurugu na fukuto la mapigano yaliozuka kwenye eneo la mashariki, katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Mapigano katika eneo hilo la nchi yalisababisha raia 250,000 kung’olewa makazi katika miezi ya karibuni, umma ambao unategemea misaada ya dharura kutoka mashirika ya kimataifa ili kukidhi mahitaji ya kimsingi. Azimio limependekeza kupelekwe wanajeshi wa kimataifa 2,785 pamoja na vikosi vya askari polisi 300. ~
Haile Menkerios, Naibu KM juu ya Masauala ya Kisiasa alisema kwenye ripoti yake mbele ya Baraza la Usalama Alkhamisi ya kuwa maafikiano kuhusu ushirikiano kwenye mpango wa amani, yaliotiwa sahihi Oktoba 25 na makundi husika na mzozo wa Usomali, yameupatia mpango huo nguvu mpya. Lakini alisema vile vile ameshuhudia kujiri mvutano na mfarakano, baina ya raisi na waziri mkuua wa Serikali ya Mpito Usomali, na anakhofia hali nchini, kwa ujumla, bado imesalia kuwa ni ya wasiwasi.
Raisedon Zenenga, Mkurugenzi wa Kitengo cha Afrika kwenye Idara ya UM juu ya Operesheni za Ulinzi wa Amani (DPKO), pia alizungumzia Baraza la Usalama na alisema utaratibu unaochukuliwa na Mataifa Wanachama kupambana na vitendo vya uharamia ni wa kupigiwa mfano, na umethibitisha aina ya hatua zinazotakikana kuchukuliwa kukabiliana na kiini cha vurugu dhidi ya usalama nchini Usomali. Alisema UM unayasihi Mataifa Wanachama kupeleka vikosi vya kimataifa katika Mogadishu, kwanza, kusawazisha hali, kitendo ambacho anaamini kitasaidia katika maandalizi ya mazingira imara yatakayouwezesha UM kupeleka vikosi vya amani baadaye kutunza usalama katika nchi nzima.
Efthimios Mitropopolous, KM wa Shirika la Kimataifa juu ya Shughuli za Bahari (IOM) alipowakilisha taarifa yake mbele ya Baraza la Usalama alisema tangu mwanzo wa 2008 hadi hivi sasa, kuliripotiwa mashambulio ya uharamia na wizi wa baharini 120 ziada, yaliotukia nje ya ya mwambao wa Usomali. Alielezea wasiwasi alionao kuhusu idadi ya marudio ya vitendo kama hivi vya uhalifu, ambavyo alisema viliendelezwa pia kwa ukatili wa hali ya juu.
Kabla ya kikao cha Baraza la Usalama kuanza majadiliano ya kuzingatia hali katika Usomali kulipitishwa na wawakilishi wa Baraza, kwa kauli moja, bila kupingwa, azimio la kukamata mali zote za wale watu waliotuhumiwa kushiriki, au kusaidia kwenye vitendo vinavyohatarisha amani, usalama na utulivu nchini Usomali.