Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Leo Baraza la Usalama lilifanyisha majadiliano ya hadhara, yalioongozwa na Raisi Oscar Arias wa Costa Rica, taifa mwenyekiti wa shughuli za Baraza kwa mwezi Novemba. Majadiliano yalizingatia namna ya kuimarisha usalama wa pamoja, kwa kuandaa sheria ya jumla itakayotumiwa kupunguza silaha na zana za vita ulimwenguni, kwa makusudio ya kusawazisha usalama na kuimarisha amani ya kimataifa.

Ripoti mpya ya KM juu ya hali Usomali, iliowakilishwa kwenye Baraza la Usalama, imebainisha dhahiri kwamba mapatano ya Djibouti bado yanasubiri kutekelezwa na makundi yanayohasimiana Usomali. Kwa hivyo, KM aliyataka makundi hayo yasipwelewe kujiunga na mpango wa amani, na kuyanasihi kuyafanya hayo bila shuruti ili, hatimaye, wafanikiwe kurudisha tena utulivu katika taifa lao. KM alisema ndani ya ripoti ya kuwa kuendelea kuharibika kwa hali ya usalama, hasa kwenye maeneo ya kusini-kati nchini Usomali, kunatishia kusambaratisha, sio juhudi za upatanishi pekee, bali pia huduma za kupeleka misaada ya kihali na kiutu nchini humo. Ripoti ilisisitiza vikosi vya ulinzi amani vya Umoja wa Afrika katika Usomali vinastahiki kuungwa mkono, na kupatiwa misaada maridhawa ya kimataifa. Aliongeza kusema, jumuiyaya kimataifa itawajibika kufungamanisha vurugu liliopo nchini kwa sasa na uwezo wa vikosi vya Umoja wa Afrika kusawazisha amani, operesheni zinazoendelea za uharamia na uwezekano wa kupeleka wanajeshi wa UM kuongoza juhudi za kukabiliana na vyanzo vya uhalifu, uvunjaji sheria na taathira zake katika Usomali. Ilivyokuwa hali ilivyo sasa hivi hairuhusu operesheni za UM kuanzishwa Usomali, kutokana na bayana hii KM alipendekeza Mataifa Wanachama, kwanza, kuchangisha vikosi vya kulinda amani vya kimataifa, fedha na zana pamoja na vifaa vya kijeshi kabla ya kupeleka wanajeshi wa UM kumudu amani kwenye eneo hilo.

Ijumanne, KM alimpigia simu Waziri Mkuu Ehud Olmert wa Israel, kutokea Geneva, kuelezea wahka mkuu alionao juu ya taathira mbaya za kimaisha zilizowabana wakazi wa Tarafa ya Ghaza. Alimsihi Waziri Mkuu, kwa kauli nzito kabisa, kuruhusu vifaa vinavyohitajika kuhudumia, kidharura, hali za umma wa Ghaza pamoja na watumishi wa UM waliopo huko. Olmert alishtumu kuendelea kwa mashambulio ya makombora ya kienyeji katika Israel, kutokea Ghaza, na alisema atazingatia ombi la dharura la KM. Kwenye ardhi iliokaliwa kimabavu kwenye Tarafa ya Ghaza, vikwazo vinaendelea dhidi ya kuingiza vifaa vinavyohitajika kukidhi mahitaji ya umma, ikichanganyika na bidhaa za biashara pamoja na nishati, vitu ambavyo pia vimepigwa marufuku kuingizwa huko, kwa mujibu wa Ofisi ya Mratibu Maalumu wa UM juu ya Mpango wa Amani kwa Mashariki ya Kati. Halkadhalika, kuanzia Alkhamisi ya tarehe 20 Novemba (2008) Shirika la UM la Kufarajia Misaada ya Kiutu kwa Wahamiaji wa Falastina katika Mashariki ya Karibu (UNRWA) limeripoti kuwa litalazimika kusimamisha ile misaada ya fedha inayofadhiliwa watu masikini sana 98,000 katika Ghaza. Hatua hii imechukuliwa kwa sababu ya ukosefu wa sarafu ya Israel ya shekel kwenye benki za Ghaza. Kamishna Mkuu wa UNRWA, Karen AbuZayd, alipohutubia kikao cha mwaka cha UNRWA – ambacho hujumuisha wahisani wa kimataifa, serikali wenyeji wanamoishi wahamiaji wa KiFalastina, mashirika yasio ya kiserikali na pia wadau wengineo – alionya kwamba shirika lake sasa hivi linakabiliwa na kile alichokiita “mzozo mkubwa wa fedha, na hatari, unaojongelea kuibana Ghaza.”