Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Ofisa wa UNHCR anasema hifadhi ya wahamiaji duniani inaregarega

Erika Feller, Kamishna Mkuu Mdogo wa Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) aliwaambia wawakilishi kutoka mataifa 76 wa Kamati ya Utendaji ya Shirika ambayo inakutana Geneva kwa sasa, ya kwamba licha ya kupatikana mafanikio mwaka uliopita kuhusu utekelezaji wa haki za kibinadamu na kiutu za kuwapatia wahamiaji ulimwenguni hifadhi inayofaa, hata hivyo imethibitika kihakika vile vile ya kwamba idadi kubwa ya wahamiaji pamoja na wale watu wenye kuomba hifadhi ya kisiasa, katika sehemu mbalimbali za dunia bado wanaendelea kukabiliwa na utovu wa ustahamilivu dhidi yao na hunyimwa haki zao halali, pia, hali ambayo inakwenda kinyume kabisa na kanuni rasmi za kimataifa juu ya wahamiaji ambazo zinawahakikishia haki hizo. ~~

KM alaani shambulio la wanajeshi wa UNAMID Sudan

KM Ban Ki-moon amelaani vikali shambulio la kundi la watu wanaokadiriwa 40 hadi 60, waliochukua silaha dhidi ya wanajeshi wa vikosi mseto vya amani kwa Darfur vya UM na UA (UNAMID), shambulio ambalo lilifanyika Ijumatatu wakati walipokuwa katika doria kutokea Nyala na kuelekea Khor Abeche. Shambulio hilo lilisababisha kifo cha mwanajeshi mmoja kutoka Nigeria. KM ameitumia Serikali ya Nigeria mkono wa taazia pamoja na aila na marafiki wa marehemu.~~

Hapa na Pale

Kamanda Mkuu mpya wa Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani katika JKK (MONUC), Liuteni Jenerali Vincente Diaz de Villegas, aliyeanza kazi wiki iliopita, Ijumatano alikamilisha ziara ya kwanza kwenye eneo la mgogoro la Kivu Kaskazini. Alipokuwepo huko alikutana na walinzi amani wa UM pamoja na timu ya watumishi wa UM waliopo huko ambapo alielezewa, kwa kina, shughuli za kijeshi pamoja hali halisi ya usalama kieneo. Baada ya hapo Kamanda Mkuu wa MONUC alizuru vituo muhimu vya kulinda amani vya UM.

Wahamiaji wa JKK wamiminikia Sudan Kusini kukwepa waasi wa LRA

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limetuma timu ya dharura ya maofisa watatu, kutoka ofisi yao ya Juba, na kuwapeleka eneo la Yambio, katika jimbo la Equatoria ya Magharibi, Sudan Kusini, ili kufanya ukaguzi kuhusu mahitaji ya maelfu ya wahamiaji wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK) waliomiminikia huko kuanzia wiki mbili zilizopita.

Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu ahimiza hifadhi bora kwa wageni Afrika Kusini baada ya mauaji katili

Navanethem Pillay, Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu (OHCHR), amelaani vikali mauaji ya kikatili yaliotukia Ijumaaa iliopita katika kijiji cha Eastern Cape, Afrika Kusini ambapo Sahra Omar Farah, mama wa KiSomali pamoja na watoto wake wawili wa kiume wajane, ambao mmoja wao alikuwa kiziwi, na vile vile binti wake wa miaka 12 waliuawa kikatili kwa visu na marungu karibu na duka liliokuwa linaendeshwa na Msomali.

Mashambulio dhidi ya NGOs yamekithiri Chad, imeonya OCHA

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti mashambulio yamezidi dhidi ya mashirika yasio ya kiserikali (NGOs) katika Chad mashariki. OCHA imesema watumishi wingi wa mashirika yasio ya kiserikali wameondoshwa Chad kwa sababu ya hatari wanayokabiliwa nayo kimaisha. Kwa mujibu wa OCHA, mnamo miezi 10 iliopita wahudumia misaada ya kiutu kutoka mashirika hayo walishambuliwa zaidi ya mara 120.~

FAO inapendekeza marekibisho kwenye sera ya nishati ya viumbehai

Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) limetoa mwito unaoyataka Mataifa Wanachama kufanya mapitio ya dharura kuhusu sera ya kuzalisha nishati kwa kutumia viumbe hai, suala ambao linaathiri usalama wa akiba ya chakula kwenye soko la kimataifa, na kuumiza mapato ya wakulima wadogo wadogo katika nchi maskini.

Mafukara wa kimataifa wahakikishiwa misaada hakika na KM wa UM kumudu maisha

Wakati nikielekea studio KM Ban Ki-moon alikuwa na mkutano wa kila mwezi na waandishi habari wa kimataifa. Kwenye risala yake ya ufunguzi alisema mafukara na maalhakiri wa kimataifa wana haki ya kutegemea UM na Mataifa Wanachama kuwasaidia kustawisha maisha yao, licha ya kuwa ulimwengu sasa hivi umekabiliwa na matatizo ya fedha katika soko la kimataifa.

Hapa na Pale

Baraza la Usalama Ijumanne limezingatia hatari ya biashara haramu ya madawa ya kulevya katika Guinea-Bissau na katika matifa jirabi, ambayo fungu kubwa lao ndio kwanza yanafufuka kutoka kipindi kirefu cha vita vya wenyewe kwa wenyewe. Kadhalika Baraza la Usalama baada ya kusailia tatizo la uharamia kwenye mwambao wa Usomali limepitisha, kwa kauli moja, azimio linalohimiza mataifa yenye uwezo kushirikiana na Serikali ya Mpito ya Usomali kukabiliana na uharamia pamoja na wizi wa baharini wa kutumia silaha.