Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Baraza la Usalama Ijumanne limezingatia hatari ya biashara haramu ya madawa ya kulevya katika Guinea-Bissau na katika matifa jirabi, ambayo fungu kubwa lao ndio kwanza yanafufuka kutoka kipindi kirefu cha vita vya wenyewe kwa wenyewe. Kadhalika Baraza la Usalama baada ya kusailia tatizo la uharamia kwenye mwambao wa Usomali limepitisha, kwa kauli moja, azimio linalohimiza mataifa yenye uwezo kushirikiana na Serikali ya Mpito ya Usomali kukabiliana na uharamia pamoja na wizi wa baharini wa kutumia silaha.

Tarehe 08 Oktoba hutambuliwa rasmi na UM kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Maafa. Mwaka huu siku hii inaangukia mwaka wa tatu wa kumbukumbu ya Mtetemeko wa Ardhi wa 2005 uliotukia katika Asia Kusini na ambao uligharikisha eneo moja zima la Pakistan. Mkururo wa maafa kadhaa haribifu mengineyo katika mwaka huu yalibainisha ulazima wa kuandaa, kidharura, taratibu za kupunguza athari za maafa ya kimaumbile miongoni mwa maeneo yale yenye hatari ya kudhuriwa na maafa ya kimaumbile. Kimbunga Nargis kilichopiga Myanmar, Zilzala ya Wenchuan iliotokea kwenye Jimbo la Sichuan, Uchina, pamoja na mafuriko ya kihistoria yaliojiri Marekani na Bara Hindi, na ukame maututi uliotanda kwenye maeneo ya Pembeya Afrika, matukio yote haya, bila shaka, yanaonyesha kunahitajika mchango ziada katika juhudi za kimataifa za kuandaa taratibu za kunusuru maisha ya umma, kuhifadhi maendeleo ya uchumi na njia za kupata riziki. Kwa hivyo tutaona katika 2008 juhudi za kuimarisha miundombinu muhimu ya kuwakinga jamii na maafa ya kimaumbile zinaendelea kwa mwelekeo mpya ambao, safari hii, unalenga zaidi kwenye maandalizi ya kulinda mahospitali na vituo vya afya dhidi ya athari za maafa ya kimaumbile.

UNHCR imewasaidia wahamiaji robo milioni ziada wa Afghanistan - sawa na watu 251,880 - kurejea makwao kutoka mataifa jirani ya Pakistan na Iran. Wingi wa wahamiaji hawo walisema walitaka kurejea Afghanistan kwa sababu ya matatizo mamgumu waliokabiliwa nayo ya kiuchumi na kiusalama, hasa baada ya kufumka bei za chakula na mafuta ambazo walisisitiza hawakuweza kuzimudu. Wahamiaji 248,951 walirejeshwa Afghanistan kutokea Pakistan na 2,929 kutokea Iran. Shughuli za UNHCR za kurejesha, kwa khiyari, Afghanistan wahamiaji zitasimamishwa mwisho wa Oktoba kwa sababu ya majira ya baridi, na zitarudiwa tena mwezi Machi 2009. Tangu Serikali ya Taliban ilipoondoshwa 2001 wahamiaji wa KiAfghani milioni 5 ziada walisharejeshwa Afghanistan.