Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Sudan na UM kutiliana sahihi maafikiano ya kukuza maendeleo nchini

Serikali ya Sudan leo imetiliana sahihi na mashirika 18 ya UM yaliopo nchini mkataba wa miaka minne, wenye dhamira ya kulisaidia taifa hilo katika huduma za ujenzi wa amani na kwenye shughuli za utawala, uamirishaji wa taratibu za kufuata sheria pamoja na huduma za kuzalisha ajira, kuimarisha elimu na afya ya jamii.

Hapa na Pale

Raisi Omar al-Bashir wa Sudan alipozuru mji wa El Fasher katika Darfur, alipata fursa ya kukutana, kwa muda mfupi na Mjumbe Maalumu wa Pamoja kwa Darfur wa UM/UA, Rodolphe Adada pamoja na viongozi wengine wa shirika la mchanganyiko la UM-UA linalosimamia ulinzi wa amani katika Darfur (UNAMID).

Kukamatwa kwa Karadzic kwasherehekewa na UM dhidi ya uhuru wa kupona adhabu

Mnamo Ijumatatu ya tarehe 21 Julai (2008) Radovan Karadzic, aliyekuwa Raisi wa Republika Srpska wakati wa vita katika Bosnia-Herzegovina, alishikwa na watu wa usalama wa Serbia. Karadzic alikamatwa baada ya kujificha kwa muda wa miaka 13 na kukwepa sheria yakimataifa iliomshitaki katika Julai 25, 1995 kuwa alihusika na mauaji ya halaiki dhidi ya watu wasio Waserb katika Bosni-Herzegovina, ikijumuisha WaBosnia walio Waislamu na Wacroat.

Holmes kuzuru Myanmar kufuatilia huduma za kiutu

Mkuu wa UM anayehusika na misaada ya dharura, John Holmes amewasili Myanmar Ijumanne, kwa ziara ya siku tatu, kutathminia hali ya waathiriwa wa Kimbunga Nargis na maendeleo katika kufarajia misaada ya kiutu, pamoja na juhudi za Myanmar za kufufua tena huduma za kiuchumi na jamii. Baada ya kuwasili kwenye mji wa Yangon Holmes alipanda helikopta na kwenda moja kwa moja kwenye eneo la Delta la Ayeyarwardy, liliopo kusini, ambapo uharibifu mkubwa ulipofanyika mwezi Mei.mkulipotukia uharibifu mkubwa zaidi mwezi Mei kutokana na Kimbunga Nargis, tufani iliosababisha watu 138,000 ama kufariki au kupotea nchini. Shughuli za kufufua huduma za kiuchumi na jamii zinaendelea kukithiri, zikisimamiwa na mashirika kadha ya kimataifa yaliopo katika vituo sita vya Delta la Ayeyarwady. ~

HAPA NA PALE

KM ameikaribisha hatua ya utiaji sahihi wa Taarifa ya Mwafaka (MOU) kati ya makundi yaliohasimiana Zimbabwe, kwa matumaini ya kutia moyo, utaratibu ambao umeweka msingi wa makubaliano ya kuanzisha mazungumzo rasmi ya kumaliza mzozo wa kisiasa nchini. KM alimpongeza Raisi Thabo Mbeki wa Afrika Kusini na timu yake ya wapatanishi kwenye juhudi zao zilizowezesha mwafaka huo kutiwa sahihi. UM upo tayari kusaidia,kwa kila njia, kwenye jitihadi zote za upatanishi nchini Zimbabwe,alisema KM.

Wasomali waliopo Finland kusaidia maendeleo ya afya Usomali kaskazini

Tawi la Finland la Shirika la Kimataifa juu ya Wahamaji (IOM), likisaidiwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland, wameanzisha mradi mpya ujulikanao kama mpango wa Uhamaji na Maendeleo kwa Afrika (MIDA). Mradi utawahusisha Wasomali wahudumia afya 22, walio wakazi wa Finland wataalamu ambao watapelekwa Usomali Kaskazini kufanya kazi, kwa muda, na kutumia ujuzi na uzoefu wao kunyanyua sekta ya afya kimaendeleo.

Mpango wa SIT wa kupunguza malaria ulimwenguni unajadiliwa na IAEA

Shirika la UM juu ya Matumizi ya Amani ya Nishati ya Nyuklia Kimataifa (IAEA) limefanyika karibuni mkutano maalumu kwenye ofisi za UM Vienna, Austria kusailia udhibiti bora wa mbinu za kupandana za mbu dume, kwa makusudio ya kukomesha uzazi wa mayai ya mbu jike, kitendo ambacho kitatumiwa kupunguza maradhi maututi ya malaria ulimwenguni.

UNMACA imefanikiwa kufyeka mabomu 38,000 yaliotegwa Afghanistan

Haider Reza, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kufyeka Mabomu yaliotegwa ardhini Afghanistan (UNMACA) amearifu kwamba katika miezi sita iliopita kumepatikana mafanikio ya kutia moyo ambapo yaliondoshwa, kwa usalama, mabomu 38,000 yaliotegwa na kuenezwa kwenye sehemu kadha za Afghanistan. Idadi hiyo ya mabomu yaliofukuliwa ardhini na kuangamizwa inajumuisha asilimia 10 ya mabomu yote yaliofyekwa nchini humo katika miaka 18 iliopita.