Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

UNICEF yahitaji msaada wa dharura kwa waathiriwa mafuriko Namibia

UNICEF imetoa ombi linalotaka ifadhiliwe msaada wa dharura wa dola milioni 1.2 ili kufarajia misaada ya kiutu kwa watu 65,000 waliopo eneo la Namibia kaskazini, umma ambao makazi yao yaliangamizwa na mvua kali zilizonyesha katika miezi ya Januari na Februari mwaka huu. Mvua hizi zilikiuka kiwango cha kawaida na zilisababisha mafuriko yaliogharikisha mastakimu kadha wa kadha nchini humo.

Dola milioni 500 zahitajiwa na WFP kufidia mfumko wa bei ya chakula ulimwenguni

Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limetuma kwa Serikali Wanachama barua ya “ombi la dharua, na lisio la kawaida” linalopendekeza lifadhiliwe haraka dola milioni 500 mnamo wiki nne zijazo, ili kuepukana na hatari ya ulazima wa kupunguza huduma za ugawaji vyakula “kwa ule umma unaotegemea misaada hiyo kunusuru maisha”. Taarifa ya WFP imedhihirisha kukabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha na haimudu tena kununua chakula kwa sababu ya kuzuka, hivi karibuni, mfumko mkubwa wa bei za chakula katika soko za kimataifa.

'Ni dhamana ya walimwengu kuufyeka kipamoja ubaguzi', anasihi KM

Tarehe 21 Machi huadhimishwa na UM kuwa ni Siku ya Kimataifa Kuondosha Ubaguzi; na kwenye risala ya kuiheshimu siku hiyo, Katibu Mkuu Ban Ki-moon alikumbusha tena kwamba sera za ubaguzi hazijatoweka bado na zinaendelea kudhuru watu binafsi na jamii kadha wa kadha katika sehemu mbalimbali za dunia. Kwa hivyo, alizinasihi nchi zote wanachama, pamoja na makundi ya jumuiya za kiraia, halkadhalika, kuongeza juhudi zao na michango yao ili kuhakikisha tunadhibiti vyema zaidi ukabila na ubaguzi wa rangi kote ulimwenguni.

Siku ya Kupiga Vita Maradhi ya Kifua Kikuu/TB Duniani

Tarehe ya leo ya Machi 24 huheshimiwa na Umoja wa Mataifa kuwa ni Siku ya Kupiga Vita Maradhi ya Kifua Kikuu/TB Duniani. Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) thuluthi moja ya idadi ya watu ulimwenguni hivi sasa wameambukizwa na maradhi ya TB.

Suala la kudhibiti ugaidi duniani lazingatiwa tena na BU

Ijumatano Baraza la Usalama (BU) lilikutana kwenye kikao cha hadhara kuzingatia kazi za ile Kamati ya Kukabiliana na Ugaidi Duniani. Mkurugenzi Mkuu wa Kamati hiyo, Mike Smith alibainisha kwenye taarifa yake kupatikana maendeleo makubwa ya kimataifa kwenye zile juhudi za kukabiliana na vitendo vya kigaidi; na alithibitisha nchi nyingi zimefanikiwa kuingiza kwenye sheria zao za kitaifa kanuni zenye kutambua kihakika kuwa kosa la ugaidi ni jinai ya kuadhibiwa kisheria.

UM unaadhimisha Siku ya Maji Safi/Salama Duniani

Ijumamosi tarehe 22 Machi huadhimishwa kila mwaka na UM kama ni Siku ya Maji Safi na Salama Duniani, na mada ya mwaka huu inatilia mkazo huduma za usafi. Taadhima hizi ni miongoni mwa juhudi za kuamsha hisia za umma wa kimataifa kwa kukumbushana ya kuwa watu bilioni 2.6 ulimwenguni bado hawakujaaliwa uwezo wa kupatiwa usafi wa kudhibiti afya. Mwaka huu UM umeyahimiza mataifa kuongeza zile huduma za kudhibiti bora matatizo yanayosababishwa na uchafu wa makaro yenye kuharibu vyanzo vya maji safi.

Hali Usomali inajadiliwa na Baraza la Usalama

Baraza la Usalama leo linajadilia suala la Usomali kwa kusikiliza ripoti ya Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu kwa Usomali, Ahmedou Ould-Abdallah kuhusu maendeleo yaliopatikana katika wiki za karibuni katika kurudisha usalama, amani na upatanishi miongoni mwa yale makundi yanayohasimiana.

Ripoti ya KM yatathminia hali katika Usomali

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon Ijumanne aliwasilisha ripoti mpya kuhusu hali katika Usomali. Ndani ya ripoti, Katibu Mkuu alieleza kwamba timu maalumu ya mashirika ya Umoja wa Mataifa, ikiongozwa na Idara ya Umoja wa Mataifa juu ya Masuala ya Kisiasa, ilishakamilisha makadirio ya sera mpya ya Umoja wa Mataifa yenye uwazi, na inayoeleweka, kuhusu uwezekano wa kupeleka vikosi vya ulinzi wa amani vya kimataifa nchini Usomali.