Skip to main content

Ripoti ya KM yatathminia hali katika Usomali

Ripoti ya KM yatathminia hali katika Usomali

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon Ijumanne aliwasilisha ripoti mpya kuhusu hali katika Usomali. Ndani ya ripoti, Katibu Mkuu alieleza kwamba timu maalumu ya mashirika ya Umoja wa Mataifa, ikiongozwa na Idara ya Umoja wa Mataifa juu ya Masuala ya Kisiasa, ilishakamilisha makadirio ya sera mpya ya Umoja wa Mataifa yenye uwazi, na inayoeleweka, kuhusu uwezekano wa kupeleka vikosi vya ulinzi wa amani vya kimataifa nchini Usomali.

Halkadhalika, ripoti ya Katibu Mkuu imehadharisha kuwa kuna vikundi fulani kutoka nchi jirani, na pia vinavyowakilisha jamii [fulani] ya kimataifa ambavyo vimevinjari kuchochea vurugu katika Usomali, ikijumuisha mizungu ya kueneza na kupeleka silaha nchini humo. Mara nyengine vikundi hivyo huonekana kukakamaa kuitumia Usomali kama jukwaa la kulipizana kisasi na wale wenye tofauti nao kisiasa, kwa kupalilia mapigano! Ripoti ya Katibu Mkuu imelezea pia kuwepo vitendo karaha vya uharamia nchini, vitendo ambavyo, ripoti ilitilia mkazo, huathiri sana huduma za ugawaji wa misaada ya kunusuru maisha kwa umma muhitaji nchini Usomali.

Hivi sasa wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanaohusika na shughuli za kiraia na huduma za kijeshi wamepelekwa kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Afrika ambapo wanasaidia kuandaa mipango ya kuvipatia vikosi vya ulinzi wa amani vya Umoja wa Afrika (UA) katika Usomali, AMISOM, uwezo bora wa kuendesha kazi zake na kurudisha utulivu na amani ya taifa, juhudi ambazo zilipongezwa sana na Katibu Mkuu Ban Ki-moon.