Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

'Uekezaji katika shughuli za maji hufaidisha kilimo Afrika, ukitekelezwa', kusisitiza mashirika juu ya maendeleo

Taasisi tatu zinazohusika na huduma za maendeleo - yaani Benki Kuu ya Dunia, Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) na pia Taasisi ya Ushirikiano Mpya wa Maendeleo ya Afrika (NEPAD) - ambazo zinakutana hivi sasa Tunis, Tunisia kuhudhuria Wiki ya Maendeleo ya Huduma za Maji Afrika, zimetoa mwito wa pamoja unaohimiza wahisani wa kimataifa kukithirisha msaada wao wa fedha zinazohitajika, kidharura, kufadhilia Usimamizi Bora wa Matumizi ya Maji kwa Kilimo katika Afrika, hasa kwenye miradi ya kutunza maji ya mvua, udhibiti bora wa mabomba ya maji na, pia, kilimo cha umwagiliaji maji.

Mjumbe wa Tanzania anasailia ajenda ya mwaka ya KMJ

Wawakilishi wanachama wa Kamisheni juu ya Maendeleo ya Jamii (KMJ) walikusanyika karibuni kwenye Makao Makuu ya UM mjini New York kuhudhuria kikao cha mwaka, ili kuzingatia masuala anuwai yanayohusu huduma za kuimarisha maendeleo ya jamii mathalan, taratibu za kufuatwa kimataifa kukuza ajira, nidhamu ya kukimu mahitaji ya umma unaozeeka pamoja na kuzingatia yale masuala yenye kutatanisha maisha ya watu walemavu duniani.~

Mashirika ya UM yajiandaa kusaidia kihali Comoros pindi yatahitajika

Mashirika ya UM yanayohusika na misaada ya kiutu - ikijumuisha zile taasisi zinazohusika na maendeleo ya watoto, UNICEF; afya, WHO; Misaada ya Dharura, OCHA na pia usalama, UNDSS – yametangaza kipamoja kwamba yameshijiandaa kuhudumia misaada ya dharura Masiwa ya Comoros, pindi msaada huo utahitajika baada ya kuripotiwa kwamba vikosi vya Serikali, vikisaidiwa na majeshi ya Umoja wa Afrika kutokea Sudan na Tanzania walishambulia kisiwa cha Anzuwani Ijumanne, na kumwondosha raisi muasi Mohamed Bacar.

UM imetangaza huzuni kubwa kwa mauaji ya madereva wanaohudumia chakula Sudan

Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeripoti kusikitishwa na kushtushwa sana na ile taarifa iliyothibitisha madereva watatu walioajiriwa na UM Sudan kuhudumia misaada ya kiutu waliuawa hivi karibuni. Ijumamosi, dereva mmoja anayeitwa Mohamed Ali alipigwa risasi na kuuawa na washambuliaji wasiojulikana, na walimjeruhi vibaya msaidizi wake pale walipokuwa kwenye barabara inayoelekea Nyala, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kusini.

'Haiwafalii Ghana kuhamisha kwa mabavu wahamiaji wa Liberia', yanasihi UNHCR

Ofisi ya UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) imewanasihi wenye madaraka Ghana kujitahidi kusitisha haraka uhamisho wa nguvu kwa wahamiaji wa Liberia. Nasaha hii ilitangazwa baada ya Ghana kuamua Ijumapili kuwaondosha nchini wahamiaji 16 ambao walirejeshwa makwao kwa mabavu, kinyume na kanuni za kimataifa. Wingi wa wahamiaji hawa walikuwa wamesharajisiwa na UM wakisubiri kufarijiwa mahitaji yao ya kihali na UNHCR.

Bata na mpunga ndio vipengele halisi vinavyochea homa ya 'avian'

Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) limeripoti kuwa wataalamu watafiti wamethibitisha hivi karibuni kwamba chanzo halisi cha homa ya mafua ya ndege (avian) ya aina ya H5N1 hakikutokana na kuku, kama ilivyodhaniwa katika siku za nyuma, bali maradhi haya yalisababishwa na wale mabata wanaochanganyika na watu kwenye mashamba ya mpunga, hususan katika mataifa ya Thailand na Viet Nam.