Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Mazungumzo ya amani ya Uganda Kaskazini yabashiria matokeo ya kutia moyo

Wawakilishi wa Serikali ya Uganda pamoja na wale wa kundi la waasi wa LRA, wanaokutana hivi sasa katika mji wa Juba, Sudan Kusini kujadilia mamsuala ya upatanishi na amani wamekubaliana kuunda idara maalumu ya mahakama kuu itakayodhaminiwa madaraka ya kusimamia mashtaka ya watuhumiwa wa jinai ya vita viliyoshtadi nchini mwao kwa miaka ishirini na moja.

FAO itakithirisha misaada kwa waathiriwa wa mafuriko Kusini mwa Afrika

Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) limejiandaa kuongeza huduma zake kwa watu muhitaji milioni moja wanaoishi katika Malawi, Msumbiji, Zambia na Zimbabwe ambao waliathiriwa na uharibifu uliotifuliwa karibuni na mvua kali zilizozusha mafuriko yaliogharikisha mavuno na makazi. Kadhalika wapimaji wahali ya hewa wanaashiria mvua hizo zitaselelea kieneo hadi mwisho wa Machi, na wanakhofia zitauchochea Mto Zambezi kufura na kukuza uharibifu ziada kwenye maeneo husika ya kusini mwa Afrika.

UM utaisaidia Bukini kukabiliana vyema na athari za matofani

UM hivi sasa unaisadia Bukini kukabiliana na hasara kuu iliozushwa na Tufani Ivan ambayo mapema wiki hii ilipiga mwambao wa mashariki-kaskazini ya taifa hilo la Bahari ya Hindi. Bukini, ikisaidiwa na mashirika ya UM sasa wanaandaa kipamoja huduma za dharura za kuukinga umma na kimbunga kingine chenye jina la Tufani Hondo, ambayo tumearifiwa ipo njiani ikielekea eneo la mashariki.

Hapa na pale

Edward Luck, raia wa Marekani ameteuliwa kuwa Mshauri Maalumu wa KM wa UM juu ya masuala yanayohusu hifadhi-kinga na misaada ya kiutu ya dharura penye uhasama wa kitaifa.

BU kuongeza muda wa operesheni za ulinzi wa amani Usomali

Ijumatano Baraza la Usalama limepitisha, kwa kauli moja, azimio lilioidhinisha operesheni za ulinzi wa amani Usomali ziendelezwe kusimamiwa na vikosi vya AMISOM kwa miezi sita ziada. Vikosi vya AMISOM vinajumuisha wanajeshi kutoka Mataifa Wanachama wa Umoja wa Afrika na vilianza kuhudumia shughuli za amani Usomali tangu Februari 2007.

Hali katika Darfur Magharibi yazidi kuharibika

Ripoti ya KM iliyowakilishwa mbele ya Baraza la Usalama kuzingatia matayarisho ya kupeleka na kukamilisha vikosi mseto vya UM/UA kulinda amani Darfur, yaani vikosi vya UNAMID imebainisha ya kuwa hali katika Darfur Magharibi imezidi kuharibika katika miezi miwili iliopita, kitendo ambacho pia huzorotisha sana zile huduma za dharura zinazohitajika kufadhilia umma misaada ya kihali ili kunusuru maisha.

Ukiukaji wa haki za binadamu katika DRC wataharakisha MONUC

Shirika la MONUC linalohusika na Ulinzi wa Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK/DRC)limeripoti kuingiwa na wasiwasi mkuu kuhusu kuendelea kwa ukiukaji wa haki za binadamu nchini. Kwa mujibu wa taarifa za Ofisi ya MONUC inayohusika na haki za binadamu,imeeleza kwamba uchunguzi wao umethibitisha mauaji ya watu wanane, wakiwemo watoto watatu wasio hatia, yalitukia tarehe 02 Januari katika kijiji kilichopo Goma, eneo la mashariki. Kwa mujibu wa MONUC mauaji haya yaliendelezwa na askari wa Jeshi la Taifa la Kongo.

UNHCR yataka ifadhiliwe dola milioni 34 kusaidia wahamiaji wa Burundi katika Tanzania

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limetoa ombi la kutaka lifadhiliwe dola milioni 34 na jumuiya ya kimataifa kwa madhumuni ya kukamilisha mpango wa kuwapatia mastakimu ya kudumu wahamiaji 218,000 wa Burundi, wanaoishi kwenye kambi ziliopo kwenye mikoa ya Rukwa na Tabora, Tanzania tangu 1972 walipohajiri makwao kujiepusha na vurugu liliozuka nchini kutokana na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe. Ratiba ya mpango huo inazingatiwa na serikali za Tanzania na Burundi pamoja na UNHCR jkwa lengo la kusuluhisho tatizo la muda mrefu la wahamiaji wa Burundi katika Tanzania.

Aliyekuwa Waziri Rwanda akana tuhumu za mauaji ya halaiki

Ijumanne Callixte Nzabonimana, aliyekuwa Waziri wa Vijana na Michezo wa Rwanda katika 1994 alikamatwa na wernye madaraka mkoani Kigoma, Tanzania na kuhamishiwa Arusha siku hiyo hiyo Arusha kwenye magereza ya Mahakama ya UM juu ya Rwanda (ICTR). Ijumatano alipofikishwa mahakamani mbele ya Jaji Dennis Byron alikana mashtaka 11 ya kushiriki kwenye mauaji ya halaiki Rwanda mnamo 1994, pamoja na tuhumu za kuandaa mazingira ya ukatili na kuchochea raia kushiriki kwenye vitendo haramu hivyo ambavyo vilikiuka Mikataba ya Geneva juu ya Hifadhi ya Raia kwenye Vita na Mapigano.

KM ameingiwa wasiwasi kurejewa kwa mapigano Darfur Magharibi

KM Ban Ki-moon ameripoti, kwa kupitia msemaji wake, kuingiwa na wasiwasi mkubwa juu ya kurejea tena kwa mapigano, katika eneo la Darfur Magharibi la Aro Sharow, baada ya kambi ya wahamiaji wa ndani ya nchi (IDPs) iliposhambuliwa kwa mabomu kwa siku mbili mfululizo, katika tarehe 18 na 19 Februari.