Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

BU kuongeza muda wa operesheni za ulinzi wa amani Usomali

BU kuongeza muda wa operesheni za ulinzi wa amani Usomali

Ijumatano Baraza la Usalama limepitisha, kwa kauli moja, azimio lilioidhinisha operesheni za ulinzi wa amani Usomali ziendelezwe kusimamiwa na vikosi vya AMISOM kwa miezi sita ziada. Vikosi vya AMISOM vinajumuisha wanajeshi kutoka Mataifa Wanachama wa Umoja wa Afrika na vilianza kuhudumia shughuli za amani Usomali tangu Februari 2007.

Kwa mujibu wa ripoti ya Ofisi ya UM juu ya Huduma za Dharura (OCHA) serikali ya mpito ya Usomali imelipongeza pendekezo la Baraza la Usalama la kuendeleza operesheni za AMISOM kwa miezi sita ziada. Lakini hata hivyo, serikali ya mpito bado inaamini kunahitajika mchango maridhawa kutoka jumuiya ya kimataifa kufufua utulivu na amani katika nchi. Msemaji wa serikali ya Usomali, Abdi Haji Gobdon, aliarifu idara ya mawasiliano ya OCHA ya kuwa mazingira ya usalama yalivyo nchini hivi sasa yanahitajia zaidi vikosi vya ulinzi wa amani kutoka UM yenyewe, vikosi ambavyo vitakuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kijeshi na madaraka ya kutumia nguvu ili kuhakikisha mapendekezo ya Baraza la Usalama yanakamilishwa kama inavyostahiki. Alisema vikosi haba vya Umoja wa Afrika (UA) vya AMISOM viliopo Usomali sasa hivi havina uwezo wa kutuliza hali nchini kama inavyotakiwa kimataifa. Gobdon alisema ni matumaini yao kikao cha siku zijazo cha Baraza la Usalama kuzingatia suala la Usomali “kutachukuliwa uamuzi ziada wa kupeleka vikosi vya UM nchini Usomali ikiwa kweli jamii ya kimataifa imeazimu kihakika kuusaidia umma wa Usomali.”