Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Mandalizi ya UNAMID Darfur yanatathminiwa na KM

Ripoti ya KM kuhusu maendeleo katika juhudi za kuandaa vikosi vya mseto vya UM na Umoja wa Afrika (AU) vitakavyopelekwa Darfur, yaani Vikosi vya UNAMID, imebainisha kupwelewa kwa sasa kwa sababu ya kuzuka vizingiti katika kupata eneo la ardhi katika Darfur linalohitajika kujenga ofisi na makazi. Kadhalika ripoti ilisema Serekali ya Sudan bado inavuta wakati kuidhinisha ile orodha waliopelekwa ya wanajeshi wa mataifa yaliojitolea kujiunga na vikosi vya ulinzi wa amani vya UM katika Darfur vya UNAMID.

Silaha zinaendelea kumiminikia Darfur na kukiuka vikwazo vya UM

Tume ya wataalamu waliodhaminiwa na UM madaraka ya kusimamia utekelezaji wa vikwazo vya silaha dhidi ya Sudan imeripoti kugundua kwamba silaha nzito, silaha ndogo ndogo na vifaa vyengine vya kivita bado vinaendelea kupelekwa jimbo la Darfur. Vitendo hivi vinaendelezwa na Serekali ya Sudan pamoja na makundi ya waasi, hali ambayo inaharamisha vikwazo vya Baraza la Usalama dhidi ya silaha kupelekwa kwenye eneo hili la Sudan magharibi.

Mjumbe wa KM kwa Darfur aandaa mazungumzo ya upatanishi Khartoum

Wiki hii Mjumbe Maalumu wa KM kwa Darfur, Jan Eliasson alikuwa na mazungumzo na viongozi mbalimbali wa hadhi ya juu wa Serekali ya Sudan, pamoja na viongozi wa mataifa jirani ikiwa katika juhudi za kimataifa za kukamilisha matayarisho ya mkutano mkuu ujao wa kurudisha amani katika Darfur, kikao ambacho kinatarajiwa kufanyika Libya tarehe 27 Oktoba (2007).

Mahkama Maalumu Sierra Leone yatoa hukumu kwa Wanamgambo

Mahakama Maalumu kwa Sierra Leone, inayoungwa mkono kikazina UM, imepitisha hukumu ya kifungo cha miaka sita kwa Moinina Fofana, na pia kutoa adhabu ya kifungo cha miaka minane kwa Allieu Kondewa, viongozi wawili wa kundi la wanamgambo wa CDF, waliotuhumiwa kushiriki kwenye jinai ya vita pale Sierra Leone ilipokuwa imezama kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yalioshtadi kwa muda wa miaka kumi nchini.

Hapa na pale

KM Ban ameripoti kuwa ana matumaini ya kutia moyo juu ya amani kurejea katika Asia baada ya kufikiwa maafikiano ya pande sita mjini Beijing, ya kufyeka silaha za kinuklia katika Rasi ya Korea, muwafaka ulioidhinishwa na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Umma wa Korea, Uchina, Ujapani, Jamhuri ya Korea, Urusi na pia Marekani.

Walimwengu watambua mchango wa watu wazee katika maendeleo

Tarehe 01 Oktoba iliadhimishwa na UM kuwa ni ‘Siku Kuu ya Watu Wenye Umri Mrefu/Watu Wazee’ na kulitolewa mwito maalumu ulioyahimiza mataifa yote wanachama kuandaa miradi ya kizalendo, kwa dhamira ya kuwapatia umma wa kimataifa wenye umri wa miaka 60 na zaidi, wanaotafsiriwa kama watu wazee, pensheni ya kudumu maridhawa itakayowasaidia kuishi vizuri kama raia wengine wenziwao.

Baraza Kuu lakhitimisha mjadala wa mwaka na kuhimiza kuwepo vitendo badala ya maneno

Mjadala wa kikao cha 62 cha wawakilishi wote ulioshtadi katika ukumbi wa Baraza Kuu, mjini New York, kuanzia tarehe 25 Septemba, ulikamilishwa na kutiwa kikomo Ijumatano tarehe 03 Oktoba. Kabla ya mijadala kuanza wajumbe kutoka nchi 191 wanachama walitatarajiwa kuwasilisha sera zao kuhusu uhusiano wa kimataifa. Baada ya mijadala kukamilishwa wawakilishi kutoka mataifa 189 ndio waliosajiliwa kumudu kuzungumzia kikao.