Hapa na pale
KM Ban ameripoti kuwa ana matumaini ya kutia moyo juu ya amani kurejea katika Asia baada ya kufikiwa maafikiano ya pande sita mjini Beijing, ya kufyeka silaha za kinuklia katika Rasi ya Korea, muwafaka ulioidhinishwa na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Umma wa Korea, Uchina, Ujapani, Jamhuri ya Korea, Urusi na pia Marekani.
Ripoti ya UNHCR imetahadhirisha kuwa wasiwasi uliojiri karibuni kwenye mataifa mengi kuhusu usalama wa mamlaka zao ni hali inayohatarisha utekelezaji wa haki za kiutu kwa wahamiaji na wakimbizi wa kigeni ambao mara nyingi hunyimwa hifadhi ya kisiasa, kinyume na kanuni za kimataifa.
Tarehe 02 Oktoba imeadhimishwa na Baraza Kuu la UM kuwa ni 'Siku ya Kimataifa ya Kutotumia Nguvu', taadhima ambazo zilifanyika katika siku ya kuzaliwa Mohandas (Mahatma) Karamchand Gandhi, mwanaharakati wa Bara Hindi ambaye alifanikiwa kugombania uhuru wa taifa lake dhidi ya wakoloni bila ya kutumia mabavu.
Tarehe 01 Oktoba ilikuwa ni 'Siku ya Makazi Bora Duniani', na muktadha wa sherehe za mwaka huu umetilia mkazo kauli isemayo “salama ya miji ipo kwenye miji yenye haki."
Ripoti mpya ya Shirika la UM juu ya Maendeleo na Biashara (UNCTAD) imeashiria mtiririko wa uekezaji wa moja kwa moja wa vitega uchumi utaongezeka kote duniani katika miaka mitatu ijayo, licha ya kuwa bado kuna wasiwasi juu ya soko la fedha lisiokuwa na utulivu na baada ya kujiri ile sera ya kulinda viwanda vya kizalendo miongoni mwa baadhi ya mataifa.
Alkhamisi Oktoba 04, kwa mara ya kwanza tangu kubuniwa UM, Baraza Kuu lilianzisha kikao cha kihistoria cha siku mbili, cha daraja ya juu, kuzingatia hatua za kuchukuliwa kipamoja kuboresha mafahamiano mema kati ya dini na tamaduni anuai, hatua ambazo Raisi wa Baraza Kuu, Srgjan Kerim alitumai zitawahamasisha Mataifa Wanacahama kuimarisha maadili ya Mkataba wa UM ya kuheshimu utu na amani ya kimataifa kwa usawa wa wote kote duniani.