Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza Kuu lakhitimisha mjadala wa mwaka na kuhimiza kuwepo vitendo badala ya maneno

Baraza Kuu lakhitimisha mjadala wa mwaka na kuhimiza kuwepo vitendo badala ya maneno

Mjadala wa kikao cha 62 cha wawakilishi wote ulioshtadi katika ukumbi wa Baraza Kuu, mjini New York, kuanzia tarehe 25 Septemba, ulikamilishwa na kutiwa kikomo Ijumatano tarehe 03 Oktoba. Kabla ya mijadala kuanza wajumbe kutoka nchi 191 wanachama walitatarajiwa kuwasilisha sera zao kuhusu uhusiano wa kimataifa. Baada ya mijadala kukamilishwa wawakilishi kutoka mataifa 189 ndio waliosajiliwa kumudu kuzungumzia kikao.

Raisi wa Baraza Kuu Srgjan Kerim kwenye risala ya kufunga mijadala alisema asilimia kubwa ya wajumbe wa kimataifa walionesha hima ya kutaka kuchukuliwe hatua za dharura kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa duniani, hasa ilivyogunduliwa kwamba majabali ya barafu katika eneo la Arctic [kaskazini ya dunia] yameonekana kuanza kuyayuka kusiko kwa kawaida, hali ambayo inatishia kuangamiza yale mataifa ya visiwa kwa sababu ya kuzidi kwa kina cha maji kwenye bahari kuu, hali ambayo huenda ikaamsha mafuriko yasio kifani yenye uwezo wa kugharikisha maeneo ya visiwa. Bw Kerim alisema nchi nyingi zinapendelea jumuiya ya kimataifa kuratibu ramani ya dharura itakayosaidia walimwengu kukabailiana vyema na tatizo la mabadiliko ya hali hewa duniani.

KM Ban Ki-moon risala yake ilizindua kwamba mjadala wa mwaka huu ulionesha kuwa na harakati na mhemko wa kidiplomasiya mkali kabisa, na anaamini mwelekeo huu katika uhusiano wa kimataifa umeweka mizizi imara itakayoisaidia jamii ya kimataifa kusuluhisha haraka ile mizozo sugu yenye kusumbua umma wa kimataifa, hususan yale masuala yanayoambatana na vurugu la Darfur, Sudan; uhasama katika Iraq na hali inayoregarega katika Afghanistan.