Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Mjadala wa wawakilishi wote kuhitimishwa kwenye Baraza Kuu la UM

Mjadala wa wiki mbili wa wawakilishi wote kwenye Baraza Kuu la UM ulihitimishwa hapo Ijumatano kwa moyo mzito. Mjadala huu, wa kikao cha 61 cha Baraza Kuu, ulihudhuriwa na maofisa mbalimbali, wa vyeo vya juu, kutoka Serekali wanachama, maofisa ambao wingi wao walihimizana kuongezwe uangalifu wa jumla miongoni Mataifa Wanachama, ili kuhifadhi heshima na hadhi ya UM katika kazi zake.

Mahakama ya ICTR na wanadiplomasiya washauriana na Kenya utaratibu wa kumshika mtuhumiwa wa mauaji ya halaiki

Hassan Bubacar Jallow, Mwendesha Mashitaka wa Mahakama ya UM juu ya Rwanda (ICTR)amefanya mazungumzo mjini Nairobi na wawakilishi wa ofisi za ubalozi 25 pamoja na mawaziri wa Kenya, akiwemo Waziri wa Sheria, Martha Karua kuzingatia juhudi za pamoja za kumshika yule mfanya biashara mtoro wa Rwanda, Felicien Kabuga ambaye alituhumiwa kufadhilia msaada wa kuendeleza mauaji ya halaiki nchini mnamo mwaka 1994.

WFP inahitajia msaada wa dharura wa dola milioni 44 kuhudumia walioathirika na ukame Kenya

Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeripoti kuwa linahitajia kufadhiliwa, haraka iwezekanavyo, na wahisani wa kimataifa msaada wa dola milioni 44 ili kuhudumia operesheni zake nchini Kenya katika kiezi sita ijayo na kunusuru maisha ya umma ulioathirika na ukame. Ijapokuwa idadi ya watu wanaohitajia msaada wa chakula imeteremka kwa sasa, kutokana na mvua za karibuni, hata hivyo WFP bado itahitajia kupatiwa msaada wa kununua nafaka, chakula cha dharura ambacho hupendelewa zaidi na waathiriwa wa ukame.

Haki za binadamu zinaendelea kuharamishwa Sudan

Mkariri Maalumu juu ya Haki za Kiutu katika Sudan, Sima Samar katika risala yake mbele ya wajumbe wa kikao cha Baraza la UM juu ya Haki za Kiutu, ambacho kinakutana mjini Geneva, hivi sasa, alionya kwamba vikosi vya Serekali ya Sudan, pamoja na wanamgambo kadhaa, wakijumuika na makundi ya waasi na vile vile vikundi vya wapinzani kutoka taifa jirani la Chad bado wanaendelea kuharamisha haki za binadamu katika Sudan. Alisema imethibitika makundi hayo huendeleza, kihorera, mauaji ya watu ndani ya Sudan bila kujali adhabu, hususan katika jimbo la Darfur.

Jumuiya ya kimataifa kuongeza muda wa UNMEE

Azzouz Ennifar, Mwakilishi wa Muda wa KM kwa Ethiopia na Eritrea amewasilisha, hivi karibuni, ripoti inayosisitiza kwamba itakuwa ni jambo la busara kuu ikiwa jumuiya ya kimataifa itakubali kuongeza muda wa kazi za Shirika la UM linalosimamia Huduma za Amani Mipakani kati ya Ethiopia na Eritrea (UNMEE) kwa miezi sita ziada. Ennifar alibashiria hatari ya kufumka tena maafa na vurugu katika eneo hilo la mipakani UM ukishindwa “kukwamua mzoroto wa mazungumzo ya upatanishi” kati ya Ethiopia na Eritrea.

UM kutoa ripoti juu ya udhibiti wa mirando ya magaidi duniani

Ripoti mpya ya UM kuhusu suala la ugaidi duniani imepongeza ushirikiano uliojiri karibuni ambapo Mataifa Wanachama yameanza kuonesha “umoja wa kimawazo” kwenye zile juhudi za kuvinyima vikundi vya kigaidi ulimwenguni fursa ya kuvuka ile mipaka iliyokosa ulinzi imara na ambapo nyaraka bandia hutumiwa bila pingamizi.

Mukhtasari unaongaza wiki ya kwanza ya mjadala wa wawakilishi wote katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Mjadala wa kila mwaka wa wawakilishi wote kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ulifunguliwa rasmi hapo Ijumanne, tarehe 19 Septemba (2006) na Sheikha Haya Rashed Al Khalifa wa Bahrain. Sheikha Haya katika hotuba yake ya ufunguzi aliwahimiza viongozi wa kimataifa waliokusanyika kwenye Makao Makuu kulenga zaidi juhudi zao katika kutekeleza kwa vitendo ahadi zao ili kusaidia kupunguza ufukara na kuboresha maisha ya umma wa kimataifa, kwa ujumla. ~