Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Cambodia yafungua milango ya kituo chake cha kwanza cha saratani

Kituo cha Techo Santepheap katika Hospitali ya Calmette huko Phnom Penh nchini Cambodia. Picha: (Picha: N. Mokhtar / IAEA)

Cambodia yafungua milango ya kituo chake cha kwanza cha saratani

Serikali ya Cambodia leo imefungua kituo cha kitaifa cha kwanza kabisa cha ugonjwa wa saratani nchini humo. Kituo hicho cha Techo Santepheap, kilichoko katika Hospitali ya Calmette katika mji mkuu wa Phnom Penh kimejengwa kwa ushirikiano wa serikali ya Cambodia na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA).

Kituo hicho ni sehemu ya mkakati wa kitaifa na kinatarajiwa kuongeza uwezo wa nchi hiyo kupambana na mzigo unaosababishwa na ugonjwa wa saratani, kwa kuhakikisha huduma za kudhibiti ugonjwa huo kama vile za chanjo, ugunduzi wa mapema na matibabu zinapatikana.

Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Yukiya Amano, katika ufunguzi wa kituo hicho ameishukuru serikali ya Cambodia kwa kukamilisha kituo hicho, akisema  "Serikali na watu wa Cambodia wajivunie mafanikio haya makubwa kwa sababu maelfu ya wananchi watafaidika na matibabu ya kisasa ya saratani na huduma za uchunguzi na ugunduzi wa mapema katika miongo ijayo."

Kulingana na takwimu za Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Saratani, Cambodia inakabiliwa na visa vipya 15,000 vya saratani kila mwaka. Shirika hilo linasema saratani ni  moja ya magonjwa yanayosabisha vifo vingi nchini humo kufuatia ongezeko la matarajio ya maisha, mabadiliko ya maisha kama vile uvutaji sigara, kula vyakula vya mafuta mengi, pamoja na kiwango cha chini cha uchunguzi.

Mpaka leo, Cambodia ilikuwa na mashine moja tu ya matibabu ya mionzi lakini imeweka bayana mpango wa kukamilisha vituo vingine viwili vya matibabu ya mionzi na dawa za nyuklia katika miaka mitano ijayo Kaskazini na Magharibi mwa nchi hiyo.

Ugonjwa wa saratani ni changamoto ya kimataifa kiafya na kiuchumi, na serikali kote ulimwenguni zinazidi kupata shinikizo katika kukidhi mahitaji na huduma za gharama nafuu. IAEA inaendelea kushirikiana na nchi zingine zenye kipato cha chini na kati katika kukabiliana na changamoto hii.