Mashambulizi dhidi ya watoto mwaka 2017 yamekithiri- UNICEF

28 Disemba 2017

Kiwango cha mashambulizi dhidi ya watoto kote ulimwenguni ni cha kutisha wakati huu ambapo mwaka 2017 unafikia ukingoni, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF katika taarifa yake iliyotolewa leo.

John Kibego na ripoti kamili.

(Taarifa ya John Kibego)

Mjini Mosul, nchini Iraq, video ikionyesha msururu wa watoto wakiwa wameambatana na wazazi wao wakikimbia makombora. Nyuso zao zimejaa woga na hawafahamu waendako.

Taswira hii imegubika maeneo mengi duniani ambako mizozo ya kisiasa imekwapua haki za msingi za watoto za kuishi, kuendelezwa, kulindwa na kushirikishwa. Haki za kimataifa za ulinzi wa raia wakiweko watoto kwenye mizozo zikisiginwa.

image
Tarehe 30 mwezi Mei mwaka 2017, mtoto huyu ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC lakini hapa yupo ugenini, nchini Angola baada ya mapigano Kasai, DRC kulazimisha akimbie na familia yake. Elimu ni shida, usalama ni mashakani, mustakhbali wake haufahamiki.(Picha:UNICEF)

Taswira hii ya Mosul, inawakilisha Nigeria, Somalia, Yemen, Syria, Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika  ya Kati, CAR na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC bila kusahau Myanmar, msusuru wa warohingywa ukilekea Bangladesh.

Takwimu za UNICEF zinaonyesha kuwa mwaka 2017 pekee huko DRC watoto 850 walilazimika kukimbia makwao , ilhali nchini Nigeria na Cameroon Boko Haram wamesababisha watu wapatao 135 washiriki kwenye mashambulizi ya kujilipua. Nako huko CAR watoto waliuawa na hata kufanyiwa ukatili wa kingono.

Mkurugenzi wa UNICEF anayehusika program za dharura Manuel Fontaine anasema watoto wanalengwa majumbani, shuleni na kwenye viwanja vya michezo.

UNICEF inatoa wito kwa pande kinzani kwenye mzozo kuzingatia wajibu wao wa sheria za kimataifa ili kusitisha ukiukwaji wa haki dhidi ya watoto.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter