Makubaliano ya kimataifa kuhusu uhamiaji yasisahau watoto- UNICEF

30 Novemba 2017

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema makubaliano ya kimataifa kuhusu uhamiaji duniani, ni lazima yajumuishe watoto waliolazimika kuondoka makwao kutokana na sababu mbalimbali.

UNICEF imesema hiyo wakati nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wakijiandaa kukutana huko Puerto Vallarta Mexico kuanzia wiki ijayo kuandika rasimu ya makubaliano hayo, na hivyo kuhitimisha takribani mwaka mzima wa majadiliano.

Makubaliano hayo baina ya serikali yatazingatia misingi na mwenendo mzima wa uhamiaji wa kimataifa na hivyo viongozi wa dunia watatumia fursa hiyo pia kuweka ahadi za kisiasa na kifedha ili yatekelezeke.

Kwa mantiki hiyo Mkurugenzi wa programu za UNICEF Ted Chaiban amesema ni lazima viongozi hao na watunga sera wao wahakikishe uhamiaji ni salama kwa watoto.

Akinukuu ripoti ya shirika hilo iliyotolewa kabla ya mkutano huo, Bwana Chaiban ametaja mifano ya nchi ambazo tayari zimechukua hatua kuhakikisha ulinzi wa watoto hata pale wanapokuwa wanavuka mipaka.

Ametolea mfano wa nchi za Afrika Magharibi pamoja na Uganda na Ujerumani bila kusahau Sudan Kusini na Afghanistan ambako zimechukua hatua kulinda watoto wahamiaji na wanaosaka hifadhi.

image
Mtoto Feizia akiwa katika kituo cha kujifunza kwenya kambi ya wakimbizi wa ndani nchini Afghanistan, kituo kilichowezekana kutokana na usaidizi wa UNICEF. (Picha:Unicef Video capture)

UNICEF inasisitiza mambo sita ikiwemo kulinda watoto wanaosafiri bila wazazi au walezi wao, kuacha kuwaweka watoto korokoroni, na kuhakikisha watoto wote wasaka hifadhi wanapatiwa fursa ya kujifunza.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter