Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makombora yetu "hayakiuki" kanuni zozote- Korea Kaskazini

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, (wa oili kutoka kulia) akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililokutana kujadili mvutano rasi ya Korea kutokana na makombora yanayorushwa na Korea Kaskazini. (Picha:UN/Eskinder Debebe)

Makombora yetu "hayakiuki" kanuni zozote- Korea Kaskazini

Hoja ya Korea Kaskazini kuendelea kufanya majaribio ya nyuklia kinyume na makubaliano ya kimataifa imejadiliwa kwa kina leo kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wakikutana mawaziri wa mambo ya nje na mabalozi ambao nchi zao ni wajumbe wa baraza hilo.

Korea Kaskazini na Korea Kusini zilihudhuria kwa mujibu wa kanuni namba 37 ya Baraza la Usalama ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akasisitiza umoja ndani  ya chombo hicho ili hatihati ya usalama iliyopo isiongezeke.

Korea Kaskazini ijulikanayo pia kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Korea, DPRK imefanya majaribio ya makombora ya masafa marefu pamoja na nyuklia ambapo Bwana Guterres amesema..

(Sauti ya Antonio Guterres)

“Mwezi Septemba, makombora mawili aina ya Hwasong yalirushwa kupitia anga la Japan. Hakuna tahadhari yoyote ya angani au majini ilitolewa wakati wa kurushwa kwa makombora haya mawili.”

Na kama hiyo haitoshi, Bwana Guterres akasema shirika la nishati ya atomiki la Umoja wa Mataifa, IAEA bado haliruhusiwi kuingia DPRK kukagua mpango wa nyuklia wa nchi hiyo ambapo kazi ya ukaguzi inafanywa kwa kutumia picha za setilaiti. Ndipo akatoa mapendekezo yake..

(Sauti ya Antonio Guterres)

Mosi kutoegemea upande wowote, pili, kupazia sauti maadili na misingi ya suluhu ya mizozo kwa njia ya diplomasia na sheria za kimataifa na tatu ni kutoa fursa za mawasiliano baina ya pande zote.”

image
Mwakilishi wa kudumu wa Korea Kaskazini au DPRK kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Ja Song Nam akihutubia wajumbe wa Baraza la Usalama. (Picha:UN/Eskinder Debebe)
Mwakilishi wa kudumu wa DPRK kwenye Umoja wa Mataifa Balozi  Ja Song Nam akasema..

(Sauti ya Balozi Ja Song Nam)

“Msimamo wa Korea Kaskazini kuhusu mpango wa nyuklia hauwezi kuwa umekiuka sheria au kanuni yoyote ya kimataifa. Kwa njia yoyote ile Korea Kaskazini ilijitoa kwenye mkataba wa kudhibiti kuenea kwa silaha, NPT katika njia inayoridhisha..”

Marekani iliwakilishwa na Waziri wake wa Mambo ya Nje Rex Tillerson ambaye madhara ya makombora yanayorushwa na Korea Kaskazini..

(Sauti ya Rex Tillerson)

“Kuvuka anga la taifa lingine huru Japan na kutishia usalama wa anga kwa sababu haya majaribio yanafanyika bila taarifa yoyote ya awali, wao wanajibika kwa mvutano huu na hivyo wanapaswa kuwajibika na ndio wanaweza kutatua mvutano huu.”

Tarehe 19 Januari 2003, Korea Kaskazini ilitangaza kuwa inajitoa kwenye mkataba wa kudhibiti kuenea kwa silaha, NPT na kwamba kwa hatua hiyo haitawajibika tena kuzingatia vigezo vya usalama wa nyuklia vinavyotolewa na na IAEA.

image
Waziri wake wa Mambo ya Nje Rex Tillerson akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. (Picha:UN/Eskinder Debebe)