Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa fursa wachochea vijana kuwa mamluki- Guterres

Ukosefu wa fursa wachochea vijana kuwa mamluki- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema suala la ukosefu wa ajira hivi sasa siyo tu janga kwa vijana pekee bali pia ni janga kwa usalama duniani.

Bwana Guterres amesema hayo wakati akihutubia huko Lisbon, Ureno kwenye jukwaa la kujadili mikakati ya maendeleo mwaka huu likiangazia jinsi ya kuweka mikakati ya kufanikisha ajenda 2030 ya malengo ya maendeleo endelevu.

(Sauti ya Guterres)

“Katika tafiti za hivi karibuni kuhusu wapiganaji mamluki ambao wako huko Iraq, Syria na kwingineko kwenye mizozo, ilibanika kuwa chanzo kikuu cha vijana hawa kujitumbukiza kwenye shughuli hizo ni ukosefu wa fursa kwenye nchi zao wenyewe.”

Halikadhalika Katibu Mkuu akaoanisha utekelezaji wa ajenda 2030 na mabadiliko ya tabianchi sambamba na mienendo ya uhamiaji akisema..

(Sauti ya Guterres)

"Hakutakuwepo na mafanikio ya ajenda 2030 iwapo mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi hautatekelezwa kwa ukamilifu wake. Huo ni mtazamo wangu. Pili hakutakuwepo na mafanikio ya ajenda 2030 iwapo hatutakuwa na mjadala wa kina kuhusu mwelekeo wa idadi ya watu, hamahama ya watu, uhamiaji na iwapo hatutajadili masuala haya kiutu.”