Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uwazi utasaidia kuondoa shuku juu ya silaha za maangamizi- Guterres

UM yapinga matumizi ya silaha za nyuklia. Picha: UM

Uwazi utasaidia kuondoa shuku juu ya silaha za maangamizi- Guterres

Tishio la matumizi ya silaha za maangamizi linaongezeka kila uchao licha ya juhudi za kimataifa za kudhibiti na hatimaye kutokomeza matumizi ya silaha hizo.

Amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wakati akihutubia kikao cha ngazi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichofanyika leo New York, Marekani kuangazia mbinu za kujengeana imani ili kuondoa silaha hizo.

Guterres amesema dunia hivi sasa ina wasiwasi kuwa penginepo silaha za nyuklia zinaweza kutumiwa, hofu ambayo iko kiwango cha juu zaidi tangu kumalizika kwa vita baridi.

(Sauti ya Antonio Guterres)

“Hali kwenye rasi ya Korea iko tete zaidi na inahatarisha zaidi amani na usalama na kuleta changamoto kwenye dunia ya sasa. Bado nina wasiwasi juu ya ongezeko la makabiliano ya kijeshi na madhara yasiyofikirika yanayoweza kutokea.”

Hata hivyo Guterres amesema anatiwa moyo na umoja miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu suala la Korea Kaskazini na majaribio ya makombora ya nyuklia.

Katibu Mkuu amezungumzia pia shuku na shaka zinazoendelea kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran akisema..

(Sauti ya Antonio Guterres)

“Kwa kuongeza uelewa wa misimamo ya watu wengine na kuruhusu ubadilishanaji wa taarifa, mathalani kuhusu bajeti za kijeshi, mitazamo ya kimkakati  na mienendo ya majeshi, kunaweza kusaidia kupunguza mvutano na kuepusha mzozo.”

Bwana Guterres amesema ni matumaini yake kuwa Umoja wa Mataifa unweza kuwa na dhima kuu katika kusaidia nchi wanachama kuendeleza, kupanua na kusaidia mikakati ya kujengeana imani katika harakati za kudhibiti na hatimaye kutokomeza silaha za maangamizi.