Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Papa Francis ataka jitihada zaidi ili kutokomeza njaa

Papa Francis ataka jitihada zaidi ili kutokomeza njaa

Wakati wa ziara yake ya kwanza kwenye Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Mkuu wa Kanisa Katoliki, Papa Francis, ametangaza uungaji wake mkono lengo la maendeleo endelevu la kutokomeza njaa, akiwapongeza wafanyakazi wa shirika hilo, wakiwemo waliopoteza maisha wakiwa kazini.

Papa Francis amewasihi wafanyakazi wa WFP na bodi ya utendaji mjini Roma wasivunjike moyo au kukatizwa tamaa na matatizo, akisema anawaunga mkono kikamilifu katika kutekeleza lengo la kutokomeza njaa.

Alipowasili kwenye makao makuu ya WFP, Papa Francis alionyeshwa bamba la kumbukizi lililoandikwa majina ya wafanyakazi wa WFP waliouawa wakiwa kazini, akisema ni ushahidi wa kujitoa kwa wafanyakazi hao katika mazingira magumu, ili watu wengine wasifariki kwa njaa.

Amesema WFP ni mfano wa jinsi ya kufanya kazi kote duniani kutokomeza njaa, kupitia uratibu bora wa rasilmali za watu na mali kwa kuimarisha jamii mashinani.