Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban kuitisha kikao cha usaidizi wa kibinadamu Sahara Magharibi

Ban kuitisha kikao cha usaidizi wa kibinadamu Sahara Magharibi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon aliyeko ziarani Algeria Jumapili amekuwa na shughuli mbali mbali ikiwemo mazungumzo na Rais Abdelaziz Bouteflika na Waziri wa Mambo ya nje Ramtane Lamamra.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mazungumzo hayo na Rais Bouteflika Ban ameshukuru Algeria kwa mchango wake katika masuala ya amani na utulivu kwenye eneo hilo.

Halikadalika amepongeza marekebisho ya katiba ya Algeria yaliyotangazwa Februari Saba mwaka huu akisema huo ni mwanzo wa marekebisho nchini humo huku akigusia vijana.

“Nafikiria zaid ikuhusu umuhimu wa kuwekeza kwa vijana wa Algeria. Vijana wana nguvu na ari. Wamerithi utamaduni wa nchi hii. Natumai watakuwa na fursa ambayo ni haki yao ya kuunda mustakhbal wao.”

Ban na Waziri wa Mambo ya nje wameangazia pia masuala ya Libya, Mali na Sahara Magharibi.

Mathalani kuhusu Libya ameshukuru Algeria kwa kusaidia kuongoza mazungumzo chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa akisema pande zote za nje zenye ushawishi kwenye mzozo wa Libya zitumie ushawishi kuleta utulivu.

Amesema iwapo hakutakuwa na maendeleo kwenye mchakato wa kisiasa, hali ya kibinadamu itazidi kuwa mbaya, halikadhalika usalama na mashambulizi yanayofanywa na magaidi wa Daesh.

Kuhusu Sahara Magharibi amerejelea tamko lake la kuitishia kikao huko Geneva cha kusaka usaidizi wa kibinadamu ili kukidhi mahitaji ya wakimbizi wa Sahara Magharibi kufuatia madhila aliyoshuhudia.

Akiwa Algeria, Bwana Ban ametembelea pia mnara wa kumbukumbu ya mashujaa wa Maqam Ashahid mjini Algiers ambako ameweka shada la maua kuwakumbuka mashujaa waliopoteza maisha wakati wa vita vya kusaka uhuru kutoka Ufaransa.

image
Katibu Mkuu wa UM Ban Ki-moon akipanda mti wa mzeituni kwenye viwanja vya Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria. (Picha:UNIC/Algiers)
Halikadhalika alipanda mti wa mzeituni kwenye viwanja vya wizara ya mambo ya nje ya Algeria kuashiria matumaini na ustawi wa uhusiano kati ya Umoja wa Mataifa na Algeria.

Hii ni mara ya pili kwa Katibu Mkuu Ban kutembelea Algeria akiwa na wadhifa huo, mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2007 baada ya shambulio la kigaidi kwenye ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Algiers.