Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunaomba watu watujali ili nasi tuwe kama watoto wengine- Mtoto Deborah

Tunaomba watu watujali ili nasi tuwe kama watoto wengine- Mtoto Deborah

Mtoto mmoja anayeishi na virusi vya Ukimwi, VVU, nchini Burkina Faso amemuomba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon awasaidie ili waweze kuishi maisha ya kutambuliwa kama wengine wasio na virusi hivyo.

Deborah mwenye umri wa miaka 14 ni mmoja wa watoto wanaopata huduma kwenye kituo cha watoto wenye VVU katika hospitali ya St. Camille mjini Ouagadougou ambapo pamoja na kushukuru wafanyakazi wanaojitolea kuwatunza amesema bado wanakabiliwa na unyanyapaa kwingineko.

Ametolea mfano shuleni, barabarani na hata majumbani akisema huduma kama vile vipimo, dawa na matibabu vingalikuwa ni bure na vinapatikana bila kukosa hali yao ingalikuwa bora zaidi.

Kwa mantiki hiyo mtoto Deborah amesema ni matarajio yake kuwa ziara ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye kituo hicho itafungua macho kwa watu wengi zaidi kuwaonea huruma na hata kuwajali zaidi ili hatimaye nao wao wawe kama watoto wengine.

Akizungumza kwenye kituo hicho kinachopata usaidizi kutoka Umoja wa Mataifa, Ban amekaribisha hatua za serikali kusaidia baraza la taifa la kupambana na Ukimwi, akisema hatua zinahitajika zaidi ili kutokomeza kabisa Ukimwi mwaka 2030.