Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari na Picha kuelekea #WHS

Habari na Picha kuelekea #WHS

Kuelekea mkutano wa kimataifa wa masuala ya kibinadamu mwezi Mei huko Istanbul, Uturuki, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon anatembelea nchi kadhaa kuangazia ajedna yake kuhusu ubinadamu na utu. Miongoni mwa nchi alizozuru ni Sudan Kusini ambako ilikuwa ni nchi ya nne  baada ya Burundi na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na Ethiopia. Sudan Kusini imegubikwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu Disemba 2013.

 

image
Katibu Mkuu wa UM Ban Ki-moon alipotembelea shule ya msingi huko Sudan Kusini. (Picha@OCHA)
Alianzia ziara yake huko Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini ambako alitembelea shule iliyoko kwenye makazi salama ya raia, ndani ya ofisi za ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani Sudan Kusini, UNMISS. Makazi hayo yanahifadhi takribani wakimbizi wa ndani 20,000 wakiwemo wanawake, watoto na wanaume ambao wamelazimika kukimbia madhila tangu ghasia zilipuke miaka miwili iliyopita.
image
Nchini Sudan Kusini, mtoto mmoja kati ya wawili hajaandikishwa shuleni. (Picha:OCHA)
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuangazia masuala ya utu baadaye ulielekea Malakal, mji ulioko Kaskazini-Mashariki mwa nchi. Eneo hili kwa muda mrefu limekuwa kitovu cha ghasia Sudan Kusini tangu Disemba 2013 na kundi linalodhibiti mji huu limebadilika zaidi ya mara 12. Wakazi wake wamekuwa wahanga wa mashambulizi makali, wakilazimika kukimbia na kusaka hifadhi kwenye vituo vya Umoja wa Mataifa.

Wapo wapi watoto

Tarehe 17 na 18 Februari, eneo hili lilikumbwa tena na shambulio baya zaidi. Watu wapatao 25 waliuawa, ikwiemo wafanyakazi watatu wa misaada na watu wengine zaidi ya 122 walijeruhiwa.

Naibu msaidizi wa Katibu Mkuu kuhusu masuala ya kibinadamu Kyung-wha Kang, alishuhudia hali ilivyo baada ya tukio..

image
Masalia baada ya mashambulizi ya tarehe 17 na 18 Februari. (Picha@OCHA)
Picha kutoka angani ikionyesha uharibifu uliotokana na mashambulio ya tarehe 17 na 18 Februari. “Wale waliohusika na mashambulio haya lazima wawajibishwe.” Alisema Bi. Kang akiongeza kuwa “Hii haikubaliki. Mapigano lazima yakome. Watu wanaonasa katikati mwa mzozo huu lazima walindwe na watoa misaada wapatiwe ruhusa bila masharti yoyote kuwafikia wale wanaohitaji misaada na ulinzi.”
image
Mama na mwana hawajui la kufanya baada ya makazi yao kuchomwa moto. (Picha@OCHA)
Wakati wa ziara, wakazi wa eneo hilo walifanya maandamano ya kimya kimya wakitaka jamii ya kimataifa iwajibike kwa wao kushindwa kulinda usalama wao. Halikadhalika walieleza matumaini yao juu ya mkataba wa amani na maridhiano baina ya makabila mbali mbali nchini humo.